Amsterdam, Uholanzi
Aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amesema anafikiri ushindi wa timu ya Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka jana ni tukio lililopangwa kabla ili kumsaidia Lionel Messi abebe taji hilo.
Argentina ikiongozwa na Messi iliibwaga Ufaransa kwa penalti 4-2 na kubeba taji hilo ikiwa ni mara ya kwanza kwa mchezaji ambaye pia alifunga mabao mawili katika mechi hiyo.
Katika fainali hizo zilizofanyika Qatar, Novemba na Desemba mwaka jana, katika mechi ya robo fainali Argengtina iliitoa Uholanzi ikiibwaga kwenye penalti baada ya sare ya mabao 2-2.
Van Gaal ambaye alitangaza kujiuzulu mara baada ya Uholanzi kutolewa katika hatua hiyo, alisema kwamba anadhani mechi yao na Argentina ilikuwa ni mpango mchafu uliopangwa kabla.
“Sitaki kusema mengi kuhusu hilo, unapoangalia jinsi Argentina walivyofunga mabao yao na jinsi sisi tulivyofunga mabao yetu na namna wachezaji wa Argentina walivyofanya faulo na hawakuadhibiwa, hapo nafikiri mechi ilipangwa kabla,” alisema Van Gaal.
Van Gaal hata hivyo alipoombwa na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa alichokisema, alijibu kwa kifupi, “namaanisha kila kitu nilichokisema.”
Alipoulizwa kwa mara ya pili kwamba kauli yake inamaanisha kwamba ilikuwa lazima Messi abebe ubingwa wa dunia, Van Gaal (pichani chini) kwa mara nyingine alijibu kwa kifupi, “Ndio, nafikiri itakuwa hivyo.”
Katika mechi ya Argentina na Uholanzi kulikuwa na tukio lenye utata kati ya Van Gaal na Messi baada ya Messi kushangilia bao lake na kwenda moja kwa moja hadi kwenye benchi la Uholanzi na kuanza kupiga makofi karibu na Van Gaal.

Baada ya hapo, Messi pia alimfuata Van Gaal mara baada ya timu hizo kupigiana penalti na Argentina kuibuka washindi, lakini baadaye mchezaji huyo alidai kujutia kufanya jambo hilo.
Kwa upande wake nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk ambaye alicheza mechi dhidi ya Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia hakuwa tayari kumuunga mkono kocha wake kwa kauli aliyoitoa.
“Nimemsikia asubuhi hii, ukweli ni kwamba hayo ni maoni yake na kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni, mimi sina maoni yanayofanana na yake.”
