Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema anatengeneza timu ambayo kila mchezaji atakuwa na uwezo wa kufunga na sio kumtegemea mchezaji mmoja.
Gamondi ambaye timu yake imefunga mabao 10 katika mechi mbili za Ligi Kuu NBC dhidi ya KMC na JKT Tanzania alisema kuwa Yanga anayoitengeneza kila mmoja atakuwa na uwezo wa kufunga.
Kocha huyo aliyasema hayo baada ya timu yake kushinda mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, jana na kukwea mpaka kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi sita sawa na Simba na Azam zilizo nafasi ya pili na ya tatu lakini zikizidiwa kwa mabao ya kufunga.
“Namna tulivyocheza naamini watu watakuwa wamefurahi, nawapongeza sana wachezaji kwani mchezo huu tumeonesha kuwa kila mchezaji anaweza kufunga mabao,” alisema Gamondi.
Alisema mchezo ulikuwa mgumu kipindi cha kwanza kutokana na jinsi wapinzani wao walivyocheza kwa faulo nyingi na kuzuia na kwamba baada tu ya kupata bao la uongozi dakika ya 45 ilisaidia wachezaji kujiamini.
Alisema kipindi cha pili timu yake ilicheza vizuri na kila mmoja alikuwa akionesha uchu wa kutaka kufunga mabao na hatimaye wakafanikiwa kuondoka na ushindi mkubwa.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Malale Hamsini alisema mabadiliko ya wachezaji aliyoyafanya hasa kipindi cha pili yamewagharimu tofauti na matarajio waliyokuwa nayo.
“Nilifanya mabadiliko ili wachezaji wakaendelee kuminya mianya ya wachezaji wa Yanga wasipenye kisha watafute goli kwa akili lakini walijikuta wanafanya makosa na kushindwa kufanya majukumu yao vizuri.
“Ukicheza na timu kama Yanga lazima uziminye njia zao, niliwaambia tunatakiwa tutafute goli la kusawazisha kwa akili lakini matokeo yake tumeshindwa kutimiza majukumu yetu,” alisema.
Alisema walicheza na timu yenye wachezaji wengi wa kimataifa na wana uwezo kwa hiyo hawalingani hivyo wameshafanya makosa na hawana budi kwenda kujipanga upya kujiandaa na michezo mingine.
