Na mwandishi wetu
Baada ya kufunga bao lake la kwanza, mshambuliaji wa Yanga, Hafiz Konkoni amesema ameanza kuuwasha moto na atahakikisha anaifanya kazi yake kwa ubora mpaka mashabiki wa Yanga wasahau machungu ya kumpoteza Fiston Mayele.
Konkoni (pichani) alifunga bao la tatu katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC kwenye mchezo uliopigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
“Nilikuja hapa na kuangalia baadhi ya video za Mayele na kugundua hatutofautiani sana na nimejifunza mengine pia kutoka kwake sababu ni mshambuliaji mzuri na amenishawishi mengi katika kupambana, nitaendelea kupambana kuhakikisha wanamsahau Mayele,” alisema Konkoni.
Konkoni raia wa Ghana alisema ameiona ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa na kwake inamfaa kwani inamuongezea kitu katika soka lake hivyo ataendelea kujifua na kujiweka sawa kwa ajili ya kuipambania Yanga katika michuano wanayoshiriki.
Mayele aliyetimkia Pyramids ya Misri msimu huu, ameendelea kukumbukwa na mashabiki wa timu hiyo katika mechi za hivi karibuni ikionekana hakuna aliyevaa viatu vyake mpaka sasa ingawa timu hiyo inapata matokeo chanya.
Msimu uliopita licha ya Mayele kuibuka mfungaji bora wa ligi akiwa amefungana na Saido Ntibazonkiza wa Simba lakini pia aliipeleka Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako aliibuka mfungaji bora akitupia mabao saba.
