Zurich, Uswisi
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetangaza kuanza uchunguzi kuhusu kitendo cha Rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales kumpiga busu mdomoni mshambuliaji wa timu hiyo, Jenni Hermoso.
Jumapili iliyopita, Rubiales alimpiga busu la mdomoni mshambuliaji huyo wakati wachezaji na viongozi wa Hispania wakifurahia ushindi baada ya kuilaza England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC).
Taarifa ya Fifa ilieleza kuwa shirikisho hilo linaloongoza soka duniani kote litaangalia kama alichofanya Rubiales kinakwenda kinyume na sheria ya 13 ya Fifa inayohusu kanuni za nidhamu na matukio yasiyofaa na yanayokwenda kinyume na fair play.
“Fifa inasisitiza juu ya kujituma bila kusita katika kuheshimu hadhi ya kila mtu na kwa nguvu zote inalaani tabia zozote zinazokwenda kinyume na jambo hilo,” ilieleza taarifa ya Fifa kwa vyombo vya habari.
Taarifa hiyo pia ilifafanua kuwa hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote anayekwenda kinyume na maadili.
“Kumdhalilisha mtu kwa nama yoyote hasa kwa kutumia ishara au hata lugha au kufanya jambo ambalo litauweka mchezo wa soka au Fifa katika mazingira ya ukosefu wa heshima, hatua za kinidhamu zitachukuliwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Itakachofanya Fifa ni kuchunguza ili kubaini kama alichokifanya Rubiales kinakwenda kinyume na sheria namba 13 inayohusu maadili na kwenda kinyume na mienendo iliyo sahihi na kukiuka kanuni ya fair play.
Rubiales akionekana mwingi wa furaha alimpiga Jenni busu ‘zito’ mdomoni mara baada ya kukabidhiwa medali, ingawa mshambuliaji huyo aliwahi kumtetea bosi huyo wa soka akisema ni tukio lililochangiwa na hali ya furaha lakini pia alisema hakulipenda.
Baadaye Rubiales naye alitaka waliolipa tafsiri mbaya tukio hilo wapuuzwe kwani lilichangiwa na yeye kuwa mwenye furaha isiyo kifani ingawa aliibuka mara ya pili na kuomba msamaha.
Viongozi kadhaa nchini Hispania wakiongowa na Waziri Mkuu, Pedro Sanchez wamelaani tukio hilo wakisisitiza kuwa kitendo cha Rubiales kuomba msamaha hakitoshi huku wengine wakimtaka ajiuzulu.
Wakati huo huo Umoja wa Wachezaji wa Profesheno umeingilia kati ukidai kwamba alichofanya Rubiales hakikubaliki na hakiwezi kuachwa hivi hivi ni lazima hatua zichukuliwe.
