Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amefuta kwa asilimia 100 mpango wa kumsajili mshambuliaji wa PSG ya Ufaransa Kylian Mbappe ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na timu hiyo.
Mbappe hadi sasa hajawa tayari kusaini mkataba mpya na PSG licha ya kutakiwa kufanya hivyo na mabosi wa klabu hiyo hali iliyozidisha matumaini kwamba alikuwa mbioni kujiunga na Real Madrid.
Mabosi PSG walimwambia mchezaji huyo achague moja kama ni kuongeza mkataba kwa wakati huu au aondoke kwa kuwa mkataba wake wa sasa unafikia ukomo Juni mwakani na iwapo PSG haitampa mkataba mpya wakati huu, mchezaji huyo ataondoka mwakani bila ya wao kulipwa chochote.
Ancelotti alipoulizwa jana Alhamisi kuhusu mpango wa kumsajili mshambuliaji huyo alijibu kwa kifupi, “Hapana, nimefuta mpango huo kwa asilimia 100.”
Akifafanua kuhusu kauli hiyo, Ancelotti alisema anadhani kikosi chake kimetimia na wachezaji wake wanafikiria kuhusu msimu wao utakavyokuwa.
Mbappe, 24, alijikuta katika wakati mgumu wakati wa maandalizi ya msimu wa 2023-24 ulioanza hivi karibuni, kwanza aliachwa katika ziara ya bara ya Asia na baadaye kutolewa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo sababu ikiwa ni mgogoro kuhusu kusaini mkataba mpya na timu hiyo.
Mshambuliaji huyo hata hivyo baadaye alirudishwa kwenye kikosi cha kwanza kwa kile kilichoelezwa kwamba tayari yamefanyika mazungumzo ya kujenga na yenye mwelekeo chanya.
PSG mapema mwezi uliopita iliipa klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia ruhusu ya kufanya mazungumzo na Mbappe baada ya kutangaza kwamba ipo tayari kuweka rekodi mpya ya dunia kwa kumsajili mchezaji huyo kwa Pauni 259 milioni.
Mbappe alijiunga na PSG mwaka 2017 akitokea Monaco pia ya Ufaransa kwa ada ya Pauni 165 milioni na hadi sasa ana rekodi ya mabao 213 katika mechi 261.
Kimataifa Ancelotti amfuta Mbappe Real Madrid
Ancelotti amfuta Mbappe Real Madrid
Read also
