Na mwandishi wetu
Kocha wa Tanzania Prisons, Fred Minziro amesema nidhamu iliyooneshwa na wachezaji wake katika mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate imewasaidia kuondoka na pointi moja katika mechi hiyo iliyoisha kwa suluhu.
Katika mechi hiyo Prisons ilikuwa ugenini katika Uwanja wa Liti, Singida ambapo Minziro amekiri kulingana na ugumu wa mchezo pointi hiyo imekuwa halali kwao.
“Singida wana timu nzuri, wamefanya usajili mzuri, wanacheza kitimu. Tulijaribu kuwaruhusu kucheza kutoka nyuma na vijana wangu walicheza kwa nidhamu wakafanikiwa kuwadhibiti,” alisema.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Singida, Mathias Lule alisema licha ya kumiliki mpira lakini walishindwa kupata ushindi akisema huenda ni kwa sababu wamechoka wakitoka kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya JKU ambao walishinda kwa mabao 4-2.
“Tumemaliza salama mchezo wetu, tulikosea kwa sababu hatujapumzika vizuri, tulifanya kila kitu lakini haikuwa bahati yetu, tulipoteza nafasi ambazo zingetupa ushindi lakini ndio soka lilivyo,” alisema Minziro.
Alisema wataendelea kujiimarisha zaidi kwa kuwa bado ni mwanzo wa ligi, wataendelea kujipanga kwa michezo ijayo kwa kufanyia kazi mapungufu yao kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi msimu huu.
