Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Namungo, Cedric Kaze amesema wanapambana kuhakikisha wanaingiza falsafa ya namna ya kupata matokeo mfululizo na kuirejesha timu hiyo kwenye michuano ya klabu Afrika.
Namungo imeanza ligi msimu huu kwa kupoteza dhidi ya JKT Tanzania kwa bao 1-0, lakini Kaze amesisitiza wanalifanyia kazi hilo ili kuhakikisha timu hiyo inaanza kupata matokeo mfululizo.
“Malengo makubwa ya Namungo ni kurudi kucheza mechi za kimataifa na iliwahi kufanya hivyo kwa mafanikio, ni ligi ngumu sana kwa sasa, lakini nafikiri kitu kikubwa ni kujiandaa na kujua tunaenda kucheza vipi.
“Ninachofahamu unaweza kukosa matokeo leo na kesho, keshokutwa ukaanza kupata kwa mfululizo na sasa tunaingiza falsafa kwa wachezaji namna ya kucheza, kuzuia, kuishi nje ya mpira, kupumzika, kula ili uwezo wa mchezaji tuutumie ipasavyo na kupata matokeo,” alisema Kaze.
Kocha huyo raia wa Burundi alisema anaamini bado wako kwenye njia nzuri ingawa wanapaswa kuongeza ubunifu hasa kwenye pasi za mwisho za mabao, mikimbio ya wasio na mpira, namna ya kufunga ili wapate matokeo kila mchezo.
Namungo inashiriki Ligi Kuu NBC kwa msimu wa tano mfululizo, msimu wa 2019-20 ilimaliza nafasi ya nne na kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, msimu uliofuata ilimaliza nafasi ya tisa kabla ya misimu miwili iliyopita kumaliza katika nafasi ya tano.
