Na Hassan Kingu
Kocha wa zamani wa Bandari Mtwara na Yanga, Kenny Mwaisabula aliwahi kuandika makala kwenye gazeti moja la michezo na kusema kwamba angekuwa wakala, mchezaji ambaye angependa kumtafutia timu nje ya nchi ni Ibrahim Ajibu.
Alimpamba Ajibu kwa sifa kadha wa kadha akiamini ni kipaji ambacho kinahitaji kupewa nafasi, baadhi yetu kwa kile tulichosikia kupitia kalamu ya mtaalam huyo wa soka tulianza kusubiri kwa hamu.
Tulijipa matumaini ya kumuona Ajibu akitafutiwa timu nje ya nchi na mawakala pamoja na kutamba katika soka la Tanzania.
Wakati huo nakumbuka jina la Ajibu ndio lilikuwa limeanza kuchomoza nchini, siku kadhaa baadaye Ajibu akawa jina miongoni mwa majina katika klabu ya Simba.
Haukupita muda tukasikia anakwenda nje ya nchi, tena picha zikapigwa akionekana uwanja wa ndege, kwa mara nyingine tukawa na matumaini kwamba kile kilichosemwa na mtaalam kinaanza kutimia.
Siku kadhaa baadaye matumaini ya Ajibu kucheza soka nje ya nchi yakaanza kufifia na kutoweka bila majibu, tukajiaminisha kwamba ataipeperusha vyema bendera ya Simba, kweli kuna nyakati alituonesha kile tulichoambiwa lakini wakati mwingine akatukatisha tamaa.
Haukupita muda tukasikia anahamia Yanga, tukaendelea kujipa matumaini kwamba huu ni wakati mwingine wa Ajibu kuwaonesha Simba kwamba walikosea kumruhusu aende Yanga.
Yanga nako hali ikawa ile ile, hakuwa na jambo kubwa la kutisha, akajirudia zake Simba, kama kawaida yetu tukaendelea kujipa matumaini kwamba iwe isiwe, Ajibu amepata fursa nyingine kuwaonesha Yanga alichonacho.
Kwa kuwa tuliaminishana kwamba ana kipaji na mtaalam alituambia kwamba ana sifa za kwenda nje ya nchi tukajipa matumaini kwamba Yanga wangejuta kumuacha Ajibu arudi Simba.
Kwa mara nyingine hali ikawa kinyume na matarajio yetu, Ajibu hakuwa na jambo kubwa la kutuufurahisha, Simba nao yakawashinda wakamuacha aende Azam FC.
Tukaendelea kujipa matumaini kwamba huu ni wakati mwingine kwa Ajibu kuwaonesha Yanga na Simba kwamba ana kipaji na kipaji chake kingeonekana akiwa Azam FC.
Nini kilitokea, Ajibu akaendelea kuwa yule yule, Azam FC nao yakawashinda, akaelekea Sindida, Fountain Gate, sisi tuliomsikia kocha akituaminisha kwamba Ajibu ni wa kucheza nje tukaendelea kuamini katika kipaji chake.

Tukaendelea kujiambia kwamba Yanga, Simba, Azam FC watakiona kwa Ajibu akiwa Singida Fountain Gate, nini kilitokea? Ajibu akajikuta katika msimu mgumu mno, hakuna mfano, mambo yakawa magumu kwake katika timu hiyo.
Ajibu tayari ameondoka Singida Fountain Gate na kutua Coastal Union, kwangu hii naiona ni mfano wa karata ya tatu na ya mwisho kwa Ajibu baada ya hapo sitashangaa nikimuona katika mabonanza, vinginevyo afanye juhudi ya kuonesha kipaji tulichoaminishwa na Mwaisabula.
Kwa Ajibu si Mwaisabula tu, bali makocha wengi na hata wachambuzi wa soka, wakati anaibuka walimpamba na kuamini kwamba amekamilika na ana sifa zote za kuwa mwanasoka bora.
Kwa wote hao ni wazi amewakatisha tamaa na kwangu naona Ajibu sasa yuko katika karata yake ya mwisho au ya tatu, nasema hivyo kwa sababu timu za Ligi Kuu Tanzania nimezipanga makundi matatu.
Kundi la kwanza ni la Simba na Yanga, kila mchezaji nchini anapenda kupita au kucheza katika timu hizo, ni timu zenye uwezo kifedha na mtaji mkubwa wa mashabiki. Ajibu amepita kote huko.
Kundi la pili ni la Azam FC na Singida Fountain Gate nayo imeingia katika kundi hili, hazina mashabiki wengi lakini zina mtaji wa fedha kukidhi mahitaji ya msingi, kwa wachezaji walio wengi wanapoona mambo magumu Simba au Yanga, chaguo namba mbili ni Azam FC ikifuatiwa na Singida Fountain Gate. Ajibu pia huko kote amepita.
Baada ya hapo sasa ndipo zinafuata timu za Coastal na nyinginezo, ndiko alipoangukia Ajibu kwa sasa, akitoka hapo tena tunaweza kumsikia Geita Gold, Mtibwa, Sugar, Kagera Sugar, KMC na kwingineko.
Huko anaweza kwenda kwa sababu moja tu, makocha walio wengi wanaamini ana kipaji na anaweza kufanya makubwa na ndio maana hawasiti kumchukua, wanajipa matumaini kwamba atabadilika na kuwa tishio na ana uwezo wa kufanya hivyo.
Na hicho ndicho hasa kilichojitokeza alipoondoka Simba na kutua Yanga hadi kurudi tena Simba kabla ya kwenda Azam FC, Singida Fountain na sasa Coastal, kote huko watu wa benchi la ufundi, makocha na hata wapambe wanaamini ana uwezo wa kufanya maajabu.
Shabiki yeyote anaweza kujiuliza ni nini hasa kinamkuta Ajibu, matumaini yanakuwa makubwa lakini unapofika wakati wa kuonesha uwezo linatokea tatizo, matumaini yanashindikana kufikiwa.
Kwa wanaoamini katika nguvu za giza watakuwa na jibu moja tu rahisi, ‘anapigwa misumari’ unaweza usipuuze jambo hili lakini halina nafasi katika soka la kisasa.
Katika soka la kisasa kuna hoja moja kwamba Ajibu hajitumi ipasavyo, uwezo anao lakini anakwama katika kufanya bidii, kukipa nguvu kipaji chake.
Niliwahi kusikia mahali hoja ya Ajibu ikizungumzwa ikidaiwa kwama mchezaji huyo aliwahi kusema kwamba hata akikaa benchi hajali kwani mshahara unaingia, hili kama ni kweli nalo huenda ni tatizo linalomkwaza.
Sina uhakika na hili lakini matokeo yake yapo wazi, kama ni kweli mchezaji ambaye amepewa matumaini makubwa lakini akajenga imani za aina hiyo ni wazi hatopata nafasi kikosi cha kwanza cha timu anayochezea, atakosa nafasi timu ya Taifa,
Kwa hali hiyo kama kauli hii ina ukweli tumtarajie Ajibu akitoka Coastal kama alivyotoka Singida Fountain Gate, atapewa nafasi lakini hatohakikishiwa namba kama hatofanya bidii, hili ni jambo la kawaida kwa kocha anayeipenda kazi yake, atampa nafasi mchezaji anayejituma.
Katika hili Ajibu afahamu kwamba suala la uhakika wa namba Coastal pia linaweza kuwa gumu kama hatofanya bidii hasa kwa timu ambayo inanolewa na kocha wa kigeni, Mwinyi Zahera.
Zahera amekuwa na Ajibu Yanga, anamjua vizuri na pengine naye ni kama makocha, wachambuzi na watu wengine wa soka wenye matumaini kwamba Ajibu bado ana uwezo lakini hata Zahera ameshamwambia kwamba anatakiwa kuitumia vizuri nafasi aliyoipata katika kikosi cha Coastal.
Mwisho wa yote nami naendelea kujipa matumaini, naamini Ajibu anaweza kuilinda kauli ya Mwaisabula kwamba ni mchezaji mwenye sifa zote, tuendelee kusubiri huenda Coastal ikawa na Ajibu yule aliyezungumzwa na Mwaisabula na wengine wengi au akawa na maisha mengine ya mafanikio nje ya Coastal?. Nani anaijua kesho?
