Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Pyramids FC ya Misri, Fiston Mayele ameitaka Yanga SC kusahau machungu ya kupoteza mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii badala yake wahamishie nguvu zote kwenye Ligi Kuu NBC.
Mayele aliyewika akiwa Yanga kabla ya hivi karibuni kutimkia Pyramids, ameyasema hayo baada ya Yanga kupoteza mechi na mahasimu wao Simba SC kwa matuta 3-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Jumapili iliyopita.
Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita, aliandika maneno hayo katika ukurasa wa mtandao wa Instagram wa kiungo wa Yanga, Khalid Aucho akionesha kuifariji timu nzima.
“Jana imepita, muangalie ligi sasa Inshallah,” aliandika Mayele huku Aucho akimjibu kwa kumuunga mkono akiandika: “Ndio kaka.”
Mayele raia wa DR Congo amekuwa pia akikumbukwa na mashabiki wa Yanga katika mechi mbili zilizopita za Ngao ya Jamii kutokana na uhaba wa upatikanaji mabao wa timu hiyo licha ya utengenezwaji wa nafasi nyingi za kufunga.
Kabla ya kufungwa juzi, Yanga ilikuwa imetwaa ndoo hiyo mara mbili mfululizo, mara zote ikiifunga Simba kwa bao 1-0 na mabao 2-1. Mabao hayo yote ya Yanga yalifungwa na Mayele.
Tangu kutua kwa Mayele, Yanga imekusanya makombe yote ya ndani iliyoshiriki kwa misimu miwili mfululizo kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la FA (ASFC) huku msimu uliopita ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Katika michuano hiyo pia Mayele aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao saba na kuweka rekodi kwa Yanga kutoa mfungaji bora kwa mara ya kwanza pia katika historia ya michuano hiyo.
Baada ya kupoteza mchezo huo wa juzi, chini ya kocha mpya, Muargetina, Miguel Gamondi aliyerithi mikoba ya Nasreddine Nabi, Yanga sasa ina kibarua cha kuhakikisha mwisho wa msimu huu inatetea makombe yake mawili yaliyosalia.
Soka Mayele awatuliza Yanga
Mayele awatuliza Yanga
Read also
