Na mwandishi wetu
Uongozi wa Klabu ya Azam FC, umesema utazitumia klabu za Simba na Yanga ili kupata mbinu za angalau kufika hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Azam ni kati ya timu nne zitakazopeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya klabu Afrika. Simba na Yanga zinashiriki Ligi ya Mabingwa na Azam na Singida Fountain Gate zinashiriki Kombe la Shirikisho.
Akizungumza katika mahojiano na Azam Media leo asubuhi, Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria (pichani) alisema ili kufikia malengo hayo wamepanga kukutana na viongozi wa timu hizo ili kuwapa mbinu sahihi zitakazowafikisha huko.
“Tumepanga kukutana na viongozi wa timu hizo mbili ambazo zimekuwa na uzoefu wa kufika huko mara kwa mara, hapa nazizungumzia timu kama Al Ahly (Misri) lakini pia Simba na Yanga ili kutupa mbinu na njia sahihi za kutufikisha angalau hatua hiyo ya makundi,” alisema Zakaria.
Kiongozi huyo alisema safari hii wamedhamiria kufanya makubwa katika mashindano yote, ndio maana wamefanya usajili wa wachezaji wengi bora ili kufikia malengo yao bila kujali ushindani kutoka kwa timu pinzani.
Alisema baada ya kulikosa taji la Ngao ya Jamii, mikakati yao ni kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu NBC ili kubeba taji hilo msimu huu na hilo wana uhakika nalo kutokana na ubora wa timu waliyokuwa nayo ukilinganisha timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo iliyoanza kuunguruma jana Jumanne.
Azam itaanza kampeni ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kucheza na Bahir Dar Kenema ya Ethiopia Jumapili ijayo na endapo itavuka hapo inatarajiwa kukutana na Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo.
