Na mwandishi wetu
Kipa wa Simba, Aishi Manula ameeleza kufurahishwa na uongozi wa timu hiyo kwa kusajili kipa mpya kutoka nje ya Tanzania akisema hiyo itamuongezea ushindani maradufu wa kuwania namba.
Uongozi wa Simba wiki iliyopita ulimtambulisha Ayoub Lakred kuwa kipa mpya wa timu hiyo akitokea FAR Rabat ya Morocco ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.
Kipa huyo ambaye ndiye kipa tegemezi wa Simba, alisema ujio wa kipa huyo utamuongezea ari ya kupambana ili kudumu kwenye nafasi yake pindi atakaporudi uwanjani baada ya kupona majeraha ya goti.
“Sijamfuatilia sana lakini naamini ni kipa mzuri ambaye atatupa ushindani mimi na wenzangu, Ally Salim na Hussein Abel sababu tunaamini ana uzoefu mkubwa kutokana na klabu aliyotoka lakini yeye ni kipa wa kigeni lazima atakuwa na kitu cha ziada ili kucheza kikosi cha kwanza,” alisema Manula.
Manula pia alisema uzoefu alionao kipa huyo anaamini atawasaidia katika michuano ya kimataifa pia wanayotarajia kushiriki hivi karibuni na hiyo ni kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwenye michuano hiyo ambayo inatarajiwa kuanza mwezi ujao.
Alisema kwa upande wake tayari ameanza mazoezi mapesi huku akifuata maelekezo ya madaktari wa timu na atafanya hivyo kwa kipindi cha miezi miwili kabla ya kurudi uwanjani.
Kwa mujibu wa ripoti ya madaktari wa Simba, Manula anatarajiwa kurudi uwanjani mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na majukumu ya kuipigania timu yake katika mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.
