London, England
Hatimaye Chelsea imeipiga rasmi bao Liverpool kwa kumsajili kiungo Moises Caicedo kutoka Brighton kwa ada ya Pauni 100 ambayo itaongezeka na kuweka rekodi ya Uingereza kwa kufikia Pauni 115 milioni.
Nyongeza ya Pauni 15 milioni ambayo itaifanya ada hiyo kufikia Pauni 115 milioni itatokana na nafasi za kucheza atakazopata mchezaji huyo katika kikosi cha Chelsea.
Liverpool ilitangaza kumtaka mchezaji huyo na kukubali kutoa Pauni 111 milioni kabla ya Chelsea kuingilia kati na Caicedo ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa ya Ecuador kuichagua Chelsea.
Chelsea ilikamilisha usajili wa mchezaji huyo Jumapili jioni, hiyo ni baada ya ofa kadhaa za timu hiyo kukataliwa lakini hatimaye Brighton ilikubali ofa ya klabu hiyo.
“Sikufikiria mara mbili Chelsea waliponihitaji, nilifahamu kwamba nahitaji kusaini katika klabu hii, ni ndoto iliyotimia kwa mimi kuja hapa na nina hamu ya kuanza kuichezea hii timu,” alisema Caicedo.
Caicedo mwenye umri wa miaka 21, alijiunga na Brighton, Februari 2021 kwa ada ya Pauni 4 milioni akitokea klabu ya Independiente del Valle ya Ecuador.
Ada ya Caicedo ikifikia Pauni 115 milioni kama inavyotarajiwa, mbali na kuweka rekodi ya Uingereza lakini pia atakuwa ni mchezaji wa pili wa bei mbaya katika Chelsea baada ya kiungo wa Argentina, Enzo Fernandez aliyesajiliwa Januari mwaka huu kwa ada ya Pauni 107.
Kocha mpya Chelsea, Mauricio Pochettino ana kazi ya kukiimarisha kikosi cha timu hiyo baada ya mambo kuwa mabaya msimu uliopita Chelsea ikimaliza nafasi ya 12 katika Ligi Kuu England (EPL).
Chelsea ambayo imeuanza msimu mpya wa EPL kwa sare ya bao 1-1 na Liverpool, tayari imewapoteza wachezaji kadhaa tegemeo wa timu hiyo kuanzia aliyekuwa nahodha wao, Cesar Azpilicueta.
Wengine ni Kalidou Koulibaly, Mason Mount, Christian Pulisic, Ruben Loftus-Cheek, Ethan Ampadu, Pierre Emerick-Aubameyang, N’Golo Kante, Abdul Rahman Baba, Kai Havertz, Mateo Kovacic na Edouard Mendy.
