Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur, Harry Kane (pichani) ameanza na mguu mbaya kwenye timu yake mpya ya Bayern Munich baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-0 na RB Leipztig katika mechi ya Super Cup Ujerumani
Ikiwa ni saa kadhaa baada ya Bayern kukamilisha usajili wa Kane ambaye pia ni nahodha wa timu ya England kwa ada ya Pauni 86 milioni, Jumamosi hii mchezaji huyo aliingia uwanjani dakika ya 64 akitokea benchi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Alianz Arena, mashabiki wa Bayern walimpokea kwa furaha mpachika mabao huyo kwa kumshangilia lakini uwapo wake haukuizuia Leipzig kutamba.
Kane katika mehezo huo aligusa mpira mara tatu tu na hakuwa na mchango wowote wakati Dani Olmo alipoifungia Leipzig mabao matatu peke yake (hat trick) yaliyotosha kumnyima Kane taji la kwanza na klabu hiyo mpya.
Akizungumzia matokeo hayo, kocha wa Bayern, Thomas Tuchel alisema kwamba ni tatizo kubwa kwani ilikuwa kama vile hakuna chochote walichokifanya katika wiki nne zilizopita.
“Siwezi kuelezea, ni kwamba hatukuwa katika ubora wa kutosha kila eneo, sijui ni kwa nini, hakuna uhusiano kati ya hali tuliyokuwa nayo na mtazamo wetu katika mechi pamoja na kiwango chetu uwanjani,” alisema Tuchel.
Msimu uliopita katika mechi kama hiyo, Bayern iliifunga Leipzig mabao 5-3 na kubeba taji hilo ambalo safari hii Leipzig wamejibu mapigo.
