London, England
Liverpool hatimaye imekubali kumsajili kiungo wa Brighton, Moises Caicedo (pichani) kwa ada ya Pauni 111 milioni na wakati wowote kuanzia sasa mchezaji huyo atafanyiwa vipimo vya afya.
Liverpool kwa muda mrefu iliingia katika mbio za kuitaka saini ya Caicedo nyota wa Ecuador mwenye umri wa miaka 21 ambaye pia alikuwa akiwindwa na klabu ya Chelsea.
Mapema mwezi uliopita, Chelsea iliwasilisha ofa ya Pauni 80 Milioni lakini mabosi wa Brighton waliikataa ofa hiyo wakitaka zaidi pengine kwa imani kwamba hakuna klabu ambayo ingekuwa tayari kutoa fedha nyingi kwa ajili ya mchezaji huyo lakini hatimaye Liverpool imefanya hivyo.
Kitendo cha Liverpool kukubali fedha nyingi kwa ajili ya Caicedo kinaweza kushangaza wengi kwani awali klabu hiyo ilijitoa katika kuisaka saini ya kiungo Jude Bellingham aliyekuwa Borussia Dortmund kwa madai kwamba isingependa kuingia katika kutoa pesa nyingi kwa ajili ya mchezaji huyo.
Bellingham hatimaye alisajiliwa Real Madrid kwa ada inayodaiwa kufikia Pauni 115 milioni na hapo hapo Liverpool imewapoteza viungo, Jordan Henderson na Fabinho waliotimkia Saudi Arabia na huenda ndio maana ikaamua kuwekeza nguvu zote kwa Caicedo.
Caicedo alisajiliwa Brighton Februari 2021 kwa ada ya Pauni 4 milioni akitokea klabu ya Independiente del Valle ya Ecuador.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amekuwa akipambana kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu wa 2023-24 baada ya kumaliza Ligi Kuu England (EPL) msimu uliopita wa 2022-23 ikiwa nafasi ya tano na kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kimataifa Liverpool yakubali kumsajili Caicedo
Liverpool yakubali kumsajili Caicedo
Read also
