Na mwandishi wetu
Yanga na Azam FC leo Jumatano zitaumana katika mechi ya Ngao ya Jamii zikiwa na falsafa za makocha wapya, Miguel Gamondi wa Yanga na Youssouph Dabo wa Azam FC lakini gumzo kubwa zaidi ni kiungo mpya wa Azam FC, Feisal Salum aliyetua hivi karibuni akitokea Yanga.
Timu hizo zinafungua pazia la michuano hiyo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga huku kila timu ikisaka ushindi wa kuivusha kwenye fainali ya michuano hiyo.
Fei ambaye aliondoka Yanga baada ya mizozo iliohusisha maslahi ya mkataba, anaweza kupokea upinzani mkubwa kwa mashabiki wa Yanga ambao pengine wanaweza kujitahidi kumzomea ili kupunguza kasi ya uwanjani ya nyota huyo kutoka Zanzibar.
Yanga wanafahamu ubora wa mchezaji huyo ambaye katika sare ya 2-2 na Azam, aliingia akitokea benchi na mashuti yake mawili nje ya 18 yaliyolenga lango yalikuwa mabao pekee ya ukombozi kwa Yanga siku hiyo, hivyo mbali ya kupambana na wachezaji wa Yanga pia atakuwa na kibarua kingine cha kuziba masikio afanye kazi yake.
Lakini kama ilivyo kawaida ya Fei mwenye sifa ya kucheza kama kiungo mkabaji, kiungo wa kati na kiungo mshambuliaji, atapambana kufanya ‘maajabu’ uwanjani ili awike katika mechi yake ya kwanza ya mashindano akiwa na Azam na kudhihirisha kwa timu nyingine kuwa taabu yake iko palepale.
Licha ya Azam kumnyakua Yanick Bangala aliyetokea Yanga pia lakini Fei amekuwa na upekee kiuchezaji, umri na hata faida ya uzawa kulingana na tafsiri ya kipaji chake hivyo kila mmoja atataka kushuhudia miguu yake itafanya nini dhidi ya waajiri wake wa kwanza katika Ligi Kuu NBC akitokea JKU ya Zanzibar takriban miaka mitano iliyopita.
Mbali na Fei, timu hizo pia zimefanya maingizo mapya ambapo Yanga imewasajili Jonas Mkude kutoka Simba, beki Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate lakini pia beki Yao Koussi, Pacome Zouzou kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Wengine ni Skudu Makudubela kutoka Marumo Gallants, Max Zengeli kutoka Maniema na beki Gift Fred kutoka SC Villa na Hafiz Konkoni kutoka Bechem huku Azam FC ikiwaongeza winga Mgambia, Gibril Sillah, mshambuliaji Alassane Diao na beki Cheikh Sidibe kutoka Senegal.

Kabla ya mechi hiyo, Yanga imecheza mechi nne za maandalizi, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, wakaifunga Magereza Ukonga mabao 10-0, Friends Rangers mabao 4-1 na kutoka suluhu na JKU ya Zanzibar.
Azam iliyoweka kambi Tunisia walicheza michezo sita ya maandalizi, waliifunga Al Hilal mabao 2-1, wakaifunga US Monastir mabao 2-1 kabla ya baadaye kufungwa mabao 3-0 na Esperance na kisha kufungwa mabao 3-1 na Stade Tunisia.
Mechi nyingine za kirafiki ambazo Azam wameshinda ni dhidi ya Bandari ya Kenya mabao 2-0 na KMKM mabao 2-0.
Yanga wataingia kwenye mchezo wa leo kama bingwa mtetezi baada ya kushinda taji hilo kwa misimu miwili mfululizo, msimu wa 2021/22 walishinda kwa kuifunga Simba bao 1-0 na msimu wa 2022/23 waliifunga tena Simba mabao 2-1.
Mechi ya Yanga na Azam FC leo hii pia inatarajiwa kuwa ya kisasi hasa kwa Azam baada ya msimu uliopita kushindwa kuondoka na pointi tatu katika michezo mitatu waliyokutana.
Kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu NBC, walitoka sare ya mabao 2-2 kisha Yanga ikashinda kwa mabao 3-2 kwenye mchezo wa marudiano. Yanga ikaifunga tena Azam bao 1-0 kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Mkwakwani, Tanga.