Na mwandishi wetu
Agosti 6, Jumamosi, 2023 itabaki katika kumbukumbu za mashabiki wa Simba, walivyoanza kuifurahia Simba Day asubuhi kwa kulitikisa jiji la Dar hadi kuhitimisha kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Power Daynamos ya Zambia.
Gumzo tangu asubuhi
Kuanzia mida ya asubuhi, mashabiki wa Simba walionesha kila dalili za kuimaliza siku vizuri, mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam hasa kwenye matawi ya klabu hiyo furaha, hamasa na matumaini makubwa vyote vilijidhihirisha.
Wanachama na mashabiki wa timu hiyo wakiwa katika mavazi ya rangi nyekundu na nyeupe wengi wao walionekana wakiwa wamejiandaa kuelekea kwenye Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya Simba Day.
Hali hiyo ilijidhihirisha nyakati za asubuhi zaidi lakini kadri muda ulivyokwenda tukio kubwa lililofuata ni la wanachama hao kuonekana kwa makundi wakielekea vituoni kupanda mabasi hadi Kwa Mkapa.
Makundi mengine ya wanachama yalikodi magari hasa aina ya Coaster, magari hayo yalipambwa na bendera za klabu hiyo zenye maandishi mbalimbali yanayopongeza mafanikio ya klabu ya Simba na maandalizi ya msimu mpya wa 2023-24 au kukejeli matukio ya mahasimu wao Yanga.

Bodaboda, bajaji
Hapo hapo bodaboda na bajaji nazo hazikuwa nyuma, ilikuwa kawaida kuona bajaji au bodaboda zilizotoa kila ishara kwamba walikuwa ni mashabiki wa Simba wanaelekea kwa Mkapa kwenye kilele cha Simba Day.
Baadhi ya bodaboda zilitawaliwa na miziki ya singeli ambayo kwa kiasi kikubwa nyimbo zake zilikuwa za kusifia mafanikio ya klabu ya simba, ilikuwa kero kwa baadhi ya watu kwa namna nyimbo hizo zilivyoimbwa kwa sauti za juu.
Taratibu mida ya saa tisa hadi 10 utulivu ulianza kurejea mitaani, mashabiki wa Simba na wengine baadhi wa Yanga safari hii walionekana kwa makundi wakiwa kwenye televisheni.
Hii haikuwa kwenye vibanda umiza pekee au baa na klabu za starehe kama ilivyozoeleka, bali hali hiyo pia ilionekana kwenye baadhi ya maduka yaliyokuwa wazi, mashabiki wa Simba na hata wasio wa Simba walikuwa wakiangalia ‘live’ kilichokuwa kikiendelea Kwa Mkapa.
Wakati huo tayari Kwa Mkapa kumefurika mashabiki wenye jezi nyekundu na nyeupe, aliyeshuhudia hali ilivyokuwa mitaani na baadaye kwa Mkapa, atakubali kwamba ilikuwa kielelezo tosha cha namna ambavyo Simba Day ililiteka jiji la Dar kuanzia asubuhi.
Zaidi ya hilo kile kilichokuwa kikizungumzwa kwamba tiketi za Simba Day zimeisha kilianza kujidhihirisha katika mida hii kwa namna ambavyo uwanja ulifurika na kupambwa kwa rangi nyekundu na nyeupe.
Kwa Mkapa
Ukiachana na burudani ya muziki, Kwa Mkapa kulikuwa na matukio makubwa matatu, kwanza ni utambulisho wa wachezaji, pili ni ujio wa mgeni rasmi na tatu ni mechi ya Simba na Power Daynamos.
Katika utambulisho wa wachezaji, mashabiki wa Simba walipata nafasi ya kuwaona wachezaji wapya na wa zamani ambao wataiwakilisha timu hiyo katika msimu mpya wa 2023-24.

Kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu katika tukio hilo ni kile kilichoitwa sapraizi wa kipa mpya, tofauti na matarajio ya wengi kwamba kipa huyo angekuwa kutoka nje ya nchi au jina lolote kubwa, Simba imemtangaza Abel Hussein aliyekuwa KMC ambaye amejiunga na timu hiyo.
Tukio la pili ni lile ambalo baadhi ya mashabiki walilitilia shaka, nani angekuwa mgeni rasmi, je ni kweli Rais Samia Suluhu Hassan angefika katika tamasha hilo au zilikuwa mbwembwe tu zilizotengenezwa?
Jibu likapatikana baada ya kiongozi huyo mkuu wa nchi kuwasili uwanjani na kupokewa kwa shangwe kabla ya kusalimiana na wachezaji wa timu zote na viongozi, na kupiga nao picha kabla ya kukabidhiwa jezi na baadye kutoa hotuba na hivyo kuingia katika historia ya kulipamba tamasha la 15 la Simba Day.
Mechi ilivyokuwa
Simba iliandika bao la kwanza katika dakika ya tano ya mchezo huo, ni bao tamu lililofungwa na nyota mpya wa timu hiyo, Willy Onana ambaye amewathibitishia mashabiki wa timu hiyo kwamba uongozi wao haukufanya kosa kumsajili.
Onana baada ya kuinasa pasi ya Muzamir Yassin, aliambaa na mpira kabla ya kupiga shuti la kiufundi lililojaa wavuni na kuwaamsha vitini mashabiki wa Simba.
Baada ya hapo ufundi mwingi ulitawala, wachezaji wa Simba hasa Clatous Chota Chama kama kawaida yake, mara kadhaa alifanikiwa kuwafanya mashabiki wafurahie burudani ya soka lililojaa ufundi ambao pia ulishuhudiwa kufanywa na beki Inonga.
Simba mbali na wachezaji mmoja mmoja kuonesha uwezo wake, kwa ujumla walifanikiwa kuonesha ubora wa kumiliki mpira kwa muda mrefu na kufika mara kwa mara kwenye lango la Dynamos ingawa hadi mapumziko walikuwa na bao hilo hilo moja.

Kipindi cha pili, Dynamos walianza kulisakama lango la Simba na kushindwa kuzitumia vizuri nafasi mbili za wazi, ya kwanza ikipotezwa na Thomas Chideli katika dakika ya 47, Chideli akiwa karibu na kipa Ally Salim alipiga shuti lililopaa juu ya lango.
Dakika mbili baadaye, Ally Salim aliokoa mpira uliopigwa na Joshua Mutale na mpira huo kumkuta Mutale tena ambaye kwa mshangao wa wengi alipiga shuti la mguu wa kushoto ambalo si tu lilipaa juu bali alikuwa kama vile beki wa Simba anaondoa hatari kwenye lango lake.
Simba walianza kuwageuzia kibao Dynamos na katika dakika ya 75 juhudi zao zilizaa matunda kwa bao la kichwa lililofungwa na nyota mwingine mpya wa timu hiyo, Fabrice Mwamba ambaye aliunganisha krosi iliyochongwa na Saido Ntibazonkiza na hivyo kutihimisha tamasha la Simba Day jioni kwa ushindi wa mabao 2-0.
Katika kipindi hicho pia mashabiki wa Simba walipewa ladha ya soka ‘waliloli-miss’ muda mrefu kutoka kwa Luis Maquissone ambaye mara kadha alionesha maufundi lakini kubwa ni pale alipopiga krosi katika dakika ya 88 na mshambuliaji mkongwe John Bocco kujitwisha kichwani lakini alishindwa kuzifumania nyavu.