Manchester, England
Manchester United imekamilisha usajili wa straika, Rasmus Hojland (pchani kushoto) kutoka Atalanta ya Italia kwa ada ya Pauni 72 milioni na mchezaji huyo kusaini mkataba wa miaka mitano.
Hojlund raia wa Denmark mwenye miaka 20 alijiunga na Atalanta inayocheza Ligi ya Serie A nchini Italia, mwaka 2022 na hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 10 katika mechi 34 za msimu uliopita.
“Si siri kwamba nimekuwa shabiki wa klabu hii kubwa tangu nikiwa mtoto mdogo, nilikuwa na ndoto za kuja hapa nikiwa mchezaji wa Manchester United,” alisema Hojlund.
Hojlund anakuwa ni usajili wa tatu wa kocha Erik ten Hag tangu dirisha la usajili majira ya kiangazi kuanza, ameshawasajili Mason Mount kutoka Chelsea na kipa Mcameroon, Andre Onana kutoka Inter Milan ya Italia.
Hojlund pia alikuwa akiwindwa na klabu kadhaa barani Ulaya ikiwamo PSG ya Ufaransa lakini sasa ni rasmi kwamba klabu hiyo imeshamkosa straika huyo ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya Denmark.
Straika huyo hata hivyo atazikosa mechi za ufunguzi za msimu mpya wa 2023-24 utakaoanza siku chache zijazo kutokana na majeraha madogo madogo aliyoyapata wakati akiiwakilisha Atalanta katika mechi za kirafiki hivi karibuni.
“Hakika nina furaha isiyo kifani kwa kupata fursa hii ya kuifanya ndoto yangu itimie, na nina dhamira ya kulipa imani niliyooneshwa katika klabu hii, bado mapema mno katika maisha yangu ya soka lakini nipo tayari kucheza na kundi hili kubwa la wachezaji wa hadhi ya juu duniani,” alisema Hojlund.
Hojlund alianza kuonesha umahiri wa kuzifumania nyavu akiwa kwao Denmark kabla ya kusajiliwa na Sturm Graz ya Austria mwaka 2020.

Tayari nyota yake imeshaanza kung’ara timu ya Taifa ya Denmar ambayo hadi sasa ameichezea mechi sita na kufunga mabao sita katika mbio za timu hiyo kuwania kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024.
