Na mwandishi wetu
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii, kocha mkuu wa Azam FC, Youssoupha Dabo (pichani) amesema hajamfuatilia mpinzani wake Yanga kutokana na ratiba nyingine za timu hiyo.
Azam FC itaumana na Yanga kwenye mechi ya kwanza itakayochezwa Agosti 9 kwenye, Uwanja wa Mkwakani, Tanga kabla ya Simba kuvaana na Singida Fountain Gate Agosti 10, mwaka huu kwenye uwanja huohuo.
Dabo alieleza hayo akibainisha kuwa kwa sasa bado wana ratiba ya mechi za kirafiki wanazozifikiria na kuziwekea mikakati kwa ajili ya kuimarisha timu yao ikiwemo mechi yao na Bandari FC ya Kenya.
“Kinachofuata sasa katika ratiba ni mchezo wa Bandari na baada ya hapo, tutakuwa na mechi na timu nyingine katika kuweka sawa kikosi chetu, hizo ndio ratiba zilizopo, baada ya hapo sasa ndio kutakuwa na muda wa kuifikiria Yanga na kuitazama zaidi,” alisema Dabo raia wa Senegal.
Pia, kocha huyo aliusifia uwezo wa kiungo mpya wa timu hiyo aliyetokea Yanga, Yanick Bangala akieleza anachohitaji mchezaji huyo kwa sasa ni muda ili kurejea kwenye kiwango chake kutokana na kukosa nafasi ya kucheza sawasawa mwishoni mwa msimu uliopita.
Alisema yeye na benchi lake la ufundi wanaendelea kumfua kiungo huyo anayemudu pia nafasi ya beki wa kati kurejea kwenye kiwango chake stahiki.
