Na mwandishi wetu
Baada ya kuwapo kitendawili cha kipa namba moja wa Simba kwa ajili ya msimu ujao, uongozi wa timu hiyo umejinadi kuwa watafanya ‘sapraizi’ ya utambulisho wa kipa wao mpya kwenye Tamasha la Simba Day.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameeleza kwa kifupi leo Ijumaa kuwa mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kuwa na wasiwasi kwani kila kitu kipo tayari na kipa huyo atatambulishwa kwenye tamasha hilo litakalofanyika keshokutwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
“Simba tunakwenda Simba Day tukiwa na wachezaji wote wamekamilika, ikiwemo atakayekuja kuchukua nafasi ya kipa Luis Jefferson naye atatangazwa hapo, ikifika hiyo siku kila kitu kitakuwa hadharani na Wanasimba watamuona kipa wao,” alisema Ally.
Kauli ya Ally imekuja wakagti zipo habari kwamba Simba iko kwenye hatua za mwisho kumnasa kipa anayekipiga nchini Ufaransa ikielezwa jana na leo viongozi wa timu hiyo wamekuwa ‘bize’ kufanya mawasiliano nchini humo kuhakikisha wanamaliza dili hilo mapema.
Wekundu hao wamemgeukia kipa huyo ambaye anafanywa siri kubwa kwa sasa baada ya kuelezwa kumkosa kipa wa Nigeria, John Noble aliyetua Tabora United akitokea Enyimba FC.
Simba inasaka mbadala wa Aishi Manula anayetarajia kuwa nje ya uwanja wa miezi minne baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini Mei 30 mwaka huu.
Manula ambaye pia ni kipa namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania au Taifa Stars, aliumia Aprili 7, mwaka huu katika mechi ya Simba dhidi ya Ihefu iliyopigwa kwenye, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.