Las Vegas, Marekani
Kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez amesema kwamba mshambuliaji wa timu hiyo, Ousmane Dembele (pichani) anahamia PSG.
Dembele mwenye umri wa miaka 26, alijiunga na Barca mwaka 2017 akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 135 milioni na amefunga mabao 40 katika mechi 185 hadi sasa.
Leo Jumatano Dembele alikuwa mmoja wa wachezaji wa akiba wa Barca katika mechi ya kirafiki dhidi ya AC Milan iliyopigwa mjini Las Vegas na Barca kutoka na ushindi wa bao 1-0 lakini mchezaji huyo hakucheza.
“Amesema kwamba hili ni wazo lake na ameamua kuondoka, ni uamuzi wake binafsi, napenda kuwa wazi katika hilo,” alisema Xavi.
“Ameamua kuwa muwazi, hilo ni wazo lake la kwenda Paris Saint Germain (PSG) kwamba ameitwa huko na sisi hapa hatuwezi kufanya lolote na ndio maana hakucheza hii leo,” alisema.
“Inaniuma mimi kwa sababu nafikiri tumekuwa tukimuangalia vizuri hapa ili awe mwenye furaha na kuwa nasi na kuendelea kuleta tofauti katika timu yetu,” aliongeza Xavi.
Mwaka jana, Dembele alisaini mkataba wa miaka miwili na Barca na kuweka rekodi ya kutoa asisti nyingi kwenye La Liga na Desemba mwaka jana alikuwamo kwenye timu ya Ufaransa iliyofikia hatua ya fainali ya Kombe la Dunia kabla ya kubwagwa na Argentina.
Msimu uliopita wa 2022-23 ambao Barca ilibeba taji la La Liga, Dembele alikosa sehemu kubwa ya nuus ya pili ya msimu huo kutokana na majeraha ya misuli yaliyokuwa yakimkabili.