Barcelona, Hispania
Barcelona hatimaye imeruhusiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2023-24 baada ya kuwapo tishio la kufungiwa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) ikituhumiwa kumlipa fedha bosi wa waamuzi.
Machi mwaka huu Uefa ilithibitisha kuanza uchunguzi wa madai ya malipo yaliyofanywa na klabu ya Barcelona yaliyohusishwa na mpango wa klabu hiyo kutaka kubebwa na waamuzi katika mechi zao.
Barcelona ambayo ilikana tuhuma hizo, sasa itashiriki michuano hiyo lakini Uefa bado wana haki ya kutoa adhabu yoyote kwa klabu hiyo wakati wowote siku zijazo kama kutakuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Uamuzi wa Uefa kufanya uchunguzi wa sakata hilo ulikuja baada ya ofisi ya waendesha mashtaka wa mjini Barcelona kufikishiwa tuhuma hizo za jinai Machi 10 mwaka huu na kuanza kuzifanyia kazi.
Katika tuhuma hizo klabu ya Barcelona inadaiwa kumlipa Pauni 7.4 milioni makamu rais wa zamani wa Kamati ya Waamuzi, Jose Maria Negreira kupitia kampuni yake ya Dasnil 95.
Waendesha mashtaka wa Barcelona baada ya kufikishiwa tuhuma hizo walianza uchunguzi kwa kuwahusisha maofisa kadhaa wa klabu ya Barcelona kwa tuhuma za rushwa, kukosa uaminifu na kufanya biashara isiyo halali.
Katika utetezi wake Barcelona ilikiri kuilipa kampuni ya Dasnil 95 kwa ajili ya ushauri wa kitaalam na lakini si kwa lengo la kutaka kubebwa na waamuzi kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
Kampuni hiyo ilitakiwa kuandaa ripoti ya ufundi inayohusisha waamuzi kupitia mechi mbalimbali ili kulisaidia benchi la ufundi la timu hiyo na kwamba jambo hilo ni la kawaida kwa klabu profesheno.
Sakata hilo lilikuwa kubwa baada ya klabu 18 za La Liga kutoa taarifa zikielezea kuguswa na tuhuma hizo lakini Rais wa Barcelona, Joan Laporta amekuwa akiitetea kwa nguvu zote klabu yake akidai inachafuliwa.
Kimataifa Barca ruksa Ligi ya Mabingwa
Barca ruksa Ligi ya Mabingwa
Read also
