California, Marekani
Baada ya kuichapa Man United mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema timu yake imekamilika hata kama haitompata mshambuliaji Kylian Mbappe (pichani).
Katika mechi hiyo iliyopigwa juzi Jumatano, kiungo mpya wa Real Madrid, Jude Bellingham alifunga bao la kwanza ambalo pia ndilo bao lake la kwanza tangu ajiunge na timu hiyo hivi karibuni kwa ada ya Dola 115 milioni.
Bao la pili la Madrid pia lilifungwa na mchezaji mpya wa timu hiyo, Joselu aliyefunga kwa kupiga tikitaka ushindi ambao umemfanya Ancelotti kujiamini kwamba timu yake imekamilika bila hata ya Mbappe.
Ancelotti ametoa kauli hiyo ikiwa ni mara ya pili baada ya awali kunukuliwa akisema kwamba ana furaha na kikosi chake licha ya kuondoka kwa mshambuliaji wao namba 9 tegemeo wa muda mrefu, Karim Benzema na kuwapo kwa habari za Mbappe kuhusishwa na mipango ya kujiunga na timu hiyo.
“Kikosi kipo sawa, hatuwezi kuwa na tatizo na kikosi, tatizo ni pale unapokuwa na kikosi kisicho na wachezaji wenye viwango, kikosi kipo vizuri na kimekamilika,” alisema Ancelloti.
Katika kilichoonekana kuwa ni kukataa kuhusishwa na hadithi ya Mbappe ambaye klabu yake ya PSG imetangaza kumpiga bei, Ancelotti alipoulizwa kuhusu mshambuliaji huyo alijibu kwa kifupi, “swali jingine.”
Hiyo ni mechi ya pili ya kirafiki kwa Real Madrid na zote imepata ushindi, katika mechi ya kwanza iliyopigwa Jumapili iliyopita mjini California, Madrid iliichapa AC Milan mabao 3-2.
Katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, Real Madrid imeimarisha kikosi chake kwa kuwasajili, Bellingham, Fran Garcia, Arda Guler, Brahim Diaz na Joselu,.
Katika safu ya ushambuliaji ya Real Madrid baada ya Benzema kuondoka, Ancelotti amekuwa akitumia mfumo wa 4-4-2 akiwa na washambuliaji wawili ambao ni Rodrygo na Vinicius Junior.
