Na mwandishi wetu
Serikali inatarajia kutumia Sh bilioni 31 kukarabati Uwanja wa Benjamin Mkapa wa Dar es Salaam, ujenzi unaotarajia kuanza mwaka huu na kukamilika Julai, mwakani.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Pindi Chana baada ya wizara kusaini mkataba na kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya China ambao pia ndio waliojenga uwanja huo awali.
Alisema lengo la kukarabati uwanja huo ni kutaka kufikia viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na kuufanya uendelee kuwa bora.
“Kukarabati uwanja ni muhimu kwa sababu umetengenezwa muda mrefu tangu mwaka 2005 hadi leo hii, pia tutaendelea kufanya marekebisho ya viwanja vingine saba,” alisema.
Pia, Dk Chana alitoa maagizo kwa kampuni ya BCEG inayohusika na uboreshwaji huo, kuhakikisha wanatengeneza kwa kiwango bora ambacho Caf na Fifa wanahitaji kwa ajili ya michuano na mechi mbalimbali zitakazohitajika kufanyika hapo.
“Wito kwa kampuni inayotengeneza uwanja kuhakikisha wanaboresha katika viwango ambavyo Caf na Fifa wanahitaji, pia Katibu Mkuu wa Wizara (Said Yakubu) simamia kwa karibu kazi hii ili ikamilike kwa wakati na viwango sahihi,” alisema.
Naye Katibu Mkuu, Yakubu alisema uwanja huo utafanyiwa marekebisho katika eneo la vyumba vya wachezaji na eneo la waandishi, kubadilisha viti vyote vya uwanjani ambavyo vimepita muda wa matumizi kwani vilitakiwa kudumu kwa muda wa miaka saba tu.
“Tutakarabati maeneo yote ya uwanja na kuweka viti vipya 45,000 na kuongeza magoli mawili pamoja na mfumo mpya wa umeme na maji. Pia kuboresha chumba maalumu ambacho mteja utalipia gharama kubwa ukija kuangalia mechi, pamoja na kuboresha taa za uwanja ambazo sasa zipo 288,” alisema Yakubu.
Yakubu alitoa wito kwa mashabiki kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo ili isiharibike kipindi wanapokuja uwanjani kuangalia mechi.
Uwanja wa Benjamin Mkapa uliokuwa ukitambulika kama Uwanja wa Taifa ulianza kujengwa mwaka 2005 na kukamilika 2007 na una uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 ukiwa ni miongoni mwa viwanja 20 bora Afrika.