Na mwandishi wetu
Siku moja baada ya kupangwa ratiba ya mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm amesema kuwa tayari ameanza kuwachunguza wapinzani wake, JKU ya Zanzibar.
Jana Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilipanga droo iliyoonesha kuwa Singida itaanza hatua ya awali kwa kuumana na JKU na timu itakayopita hapo itapepetana na Future FC ya Misri katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo.
Pluijm ameiambia GreenSports leo Jumatano kuwa kwake haijalishi kama mpinzani anatoka karibu au mbali cha msingi ni kumfahamu vyema mpinzani unayekutana naye na kupambana naye kwa nidhamu.
“Kila mechi ni ya ushindani na tunapaswa kucheza bila ya kujali ni timu kutoka Zanzibar au wapi, sifahamu mengi kuhusu wao na sasa nimeanza kuifuatilia kufahamu ubora wao, udhaifu wao na mengine kama hayo.
“Nafikiri wepesi pekee tulionao hapo ni ukaribu wa mechi hizi mbili za hatua ya awali kwamba tutakuwa hapahapa Tanzania, hilo ndilo lenye faraja kwa sasa lakini mengine ni ushindani na tunajipanga pia dhidi ya JKU,” alisema Pluijm.
