Na mwandishi wetu
Mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika mwaka 2022, Sadio Mane amempongeza aliyekuwa winga wa Simba, Pape Sakho kwa kujiunga na timu ya Union Sportive Quevillaise ya Ligi Daraja la Pili Ufaransa.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, mshambuliaji huyo anayekipiga Beyern Munich ya Ujerumani alisema anajisikia furaha kuona ndoto za Sakho za kucheza Ulaya zimetimia.
Kwa upande wake Sakho raia wa Senegal kama ilivyo kwa Mane ambaye tayari ametambulishwa Union Sportive Quevillaise, alimshukuru Mane kwa ushirikiano aliompa na kumfanikishia kufika hapo alipo.
“Asante kaka kwa kufanikisha dili hili, nakukubali sana na siku zote utabaki kuwa mfano mzuri kwangu,” alisema Sakho ambaye naye ni mshindi wa tuzo ya bao bora la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021-22.
Sakho (pichani juu) aliyeitumikia Simba kwa misimu miwili alisema baada ya dili lake la kujiunga na timu hiyo ya Ufaransa yupo katika wakati mgumu kuagana na watu wake wa karibu lakini hakuna namna sababu mchezo wa mpira ndivyo ulivyo.
“Nimeishiwa maneno ya kusema lakini siku zote Simba itabaki kuwa familia yangu, mchezo wa soka ni mchezo wa kupanda viwango, nami nimechagua kusogea mbele kwa faida yangu binafsi,” alisema Sakho.
Mchezaji huyo pia ameushukuru uongozi wa Simba, kwa ushirikiano na upendo mkubwa waliompa tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Teungueth ya kwao na ameitakia timu hiyo mafanikio mema na kushinda mataji yote itakayoshiriki msimu ujao.
