Na mwandishi wetu
Baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Zira FK ya Azerbaijan, kocha wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesifu kiwango cha timu hiyo katika mchezo huo wa kirafiki uliopigwa Uturuki.
Simba imepata sare hiyo katika mchezo wake huo wa kwanza wa kirafiki uliopigwa jana Jumatatu katika kambi ya maandalizi waliyoweka nchini humo kwa ajili ya msimu ujao wa 2023-24.
Robertinho alisema kuwa kwa kiwango walichoonesha kikosi chake, anaamini baada ya wiki chache watakuwa wamepiga hatua nzuri mno kwa kiwango cha kupambana katika michuano muhimu inayowakabili msimu ujao ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Wameonesha vizuri namna ya kutumia mbinu na wamefanikiwa, ukitazama mpinzani wetu amemaliza kujipanga lakini sisi ndio kwanza tunaanza, nafikiri ni matokeo mazuri na muhimu zaidi kwangu na benchi la ufundi, ni kiwango kilichooneshwa na timu,” alisema Robetinho.
Kocha huyo raia wa Brazil alisema pia amefurahishwa na upana wa kikosi cha timu hiyo kilivyo kwa sasa baada ya usajili wa dirisha kubwa kwani amekuwa na machaguo mengi hata inapotokea mchezaji amepata majeraha yanayomuhitaji kwenda nje.
Simba ambayo imepania kufanya vizuri msimu ujao mpaka sasa imefanikiwa kutangaza usajili wa Che Fondoh Malone, Aubin Kramo, David Kameta, Hussein Kazi, Abdallah Khamis, Idd Chilunda, Willy Onana, Fabrice Ngoma, Luis Miquissone na kipa Jefferson Luis.
