Melbourne, Australia
Timu ya Taifa ya Nigeria imeanza na sare ya 0-0 dhidi ya Canada katika mechi yake ya kwanza ya Kundi B ya fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake zinazoendelea New Zealand na Australia.
Katika mechi hiyo, Nigeria wana kila sababu ya kujivunia matokeo hayo kwa umahiri waliouonesha ikiwamo kucheza 10 uwanjani na kipa wao, Chiamaka Nnadozie kuokoa mkwaju wa penalti.
Penalti hiyo iliyotolewa muda mfupi baada ya mapumziko ilitokana na rafu ambayo Francisca Ordega alimchezea nahodha wa Canada, Christine Sinclair ambaye ndiye aliyepiga penalti hiyo lakini Nnadozie akaokoa.
Ukiachana na penalti hiyo, Nigeria ilikutwa na majanga mengine baada ya mchezaji wake Deborah Abiodun kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Lawrance ingawa awali alipewa kadi ya njano.
Picha ya VAR ilitumika na kumfanya mwamuzi ampe mchezaji huyo kadi nyekundu hali iliyowafanya Nigeria wabaki 10 uwanjani lakini walipambana na hadi mwisho wa mchezo matokeo yakabaki 0-0 na kuwafanya Nigeria watoke uwanjani kwa furaha.
Kwa Sinclair licha ya kukosa penalti hiyo lakini anashikilia rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji waliofunga kwenye fainali tano za Kombe la Dunia sawa na Marta wa Brazil na Cristiano Ronaldo wa Ureno kwa upande wa wanaume.
Sinclair pia anashikilia rekodi ya kuifungia timu ya Canada mabao 190 katika mechi 324 alizoichezea hadi sasa lakini kwa kukosa penalti anakuwa ameshindwa kumfunga kipa mwenye umri wa miaka 18 ambaye ni mdogo kwake kwa miaka 22.
Matokeo Kombe la Dunia Wanawake 2023
Nigeria 0- 0 Canada
Hispania 3-0 Costa Rica
New Zealand 1-0 Norway
Australia 1-0 Jamhuri ya Ireland
Philippines 0-2 Switzerland
Kimataifa Nigeria yaibana Canada Kombe la Dunia
Nigeria yaibana Canada Kombe la Dunia
Read also
