Manchester, England
Klabu ya Manchester United imekamilisha usajili wa kipa Andre Onana (pichani) kutoka Inter Milan kwa ada ya Pauni 47.2 milioni na hivyo kumpata mrithi wa kipa David De Gea aliyegoma kusaini mkataba mpya.
Onana mwenye umri wa miaka 27 ambaye pia ni kipa wa timu ya Taifa ya Cameroon, amekuwa akiwindwa na klabu hiyo kwa siku za karibuni, amesaini mkataba wa miaka mitano wenye kipengele kinachompa nafasi ya kuongeza mwaka mwingine mmoja.
Baada ya kukamilika usajili huo, Onana anatarajia kwenda Marekani kuujiunga na kikosi cha Man United wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2023-24 unaoanza mapema mwezi ujao.
“Kujiunga na Manchester United ni heshima ya kipekee, nimefanya juhudi kubwa katika maisha yangu yote ili kufikia hatua hii, nimepitia vikwazo vingi katika safari hiyo,” alisema Onana.
Onana anatarajia kuwa kipa namba moja ya timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Mhispaniola De Gea ambaye ameondoka katika timu hiyo aliyoichezea kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka 12.
“Kufanya kazi Old Trafford na kulinda malengo yetu na kushiriki katika timu ni jambo jingine la kipekee, huu ni mwanzo wa safari mpya kwangu, nikiwa na wachezaji wenzangu wapya na hamasa mpya ya kupambana,” alisema Onana.
Onana aliwahi kufanya kazi na kocha wa Man United, Erik ten Hag katika klabu ya Ajax ya Uholanzi na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu Uholanzi kabla ya kufungiwa miezi tisa mwaka 2021 akihusishwa na madawa ya kuongeza nguvu.
Akiwa Inter Milan ambayo alijiunga nayo Julai mwaka jana, aliiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2022-23 lakini walishindwa kutamba mbele ya Man City waliobeba taji hilo.
