Amsterdam, Uholanzi
Kipa wa zamani wa Uholanzi na klabu ya Manchester United, Edwin van der Sar (pichani) aliyekuwa na matatizo ya damu kwenye ubongo ametolewa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU).
Van der Sar ambaye pia amewahi kuidakia timu ya Ajax ya Uholanzi alikimbizwa hospitali takriban siku 10 zilizopita akiwa mapumzikoni Croatia kabla ya baadaye kuhamishiwa katika hospitali nyingine ya kwao Uholanzi.
“Nina furaha kuwaarifu kuwa kwa sasa sipo tena ICU, ingawa bado nipo hospitali lakini natarajia kurudi nyumbani wiki ijayo ikiwa ni hatua nyingine katika kuelekea kupona,” alisema Van der Sar.
Kipa huyo ambaye ameidakia timu ya Taifa ya Uholanzi katika mechi 130, Mei mwaka huu aling’atuka katika nafasi yake ya ofisa mtendaji mkuu wa klabu ya Ajax.
Van der Sar alichukua hatua hiyo baada ya timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi na kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2009.
Aliamua kustaafu soka la ushindani mwaka 2011 baada ya kuondoka Man United na kuwa mjumbe wa bodi ya klabu ya Ajax mwaka 2012 na baadaye kuwa ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo mwaka 2016.
Akiwa Man United, aliichezea timu hiyo mechi 266 na kuisaidia kubeba mataji manne ya Ligi Kuu England (EPL) na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008 na pia amewahi kuzichezea klabu za Fulham na Juventus.
