Manchester, England
Kesi ya udhalilishaji kijinsia iliyokuwa ikimkabili winga wa zamani wa Man United, Ryan Giggs haitoendelea tena baada ya waendesha mashtaka kutangaza kujiondoa katika kesi hiyo.
Giggs alitarajia kupanda kizimbani kwa mara nyingine Julai 31 mwaka huu akituhumiwa kwa tabia za ubabe na udhalilishaji dhidi ya aliyekuwa rafiki yake wa kike, Kate Greville, makosa aliyodaiwa kuyafanya kati ya Agosti 2017 na Novemba 2020.
Sambamba na kosa hilo, Giggs pia alituhumiwa kumfanyia ubabe huo dada wa Kate aitwaye Emma baada ya kuzozana naye wakiwa nyumbani kwa Giggs jijini Manchester, tukio analodaiwa kulifanya Novemba 2020.
Giggs hata hivyo alikana makosa yote hayo baada ya kufikishwa katika mahakama ya Manchester, katika kesi ambayo iliendeshwa kwa muda mrefu lakini hitimisho lilichelewa kufikiwa.
Waendesha mashitaka hao waliieleza mahakama hiyo jana Jumanne kwamba wamefikia uamuzi wa kujiondoa katika kesi hiyo baada ya Kate Greville kutoonesha utayari wa kutoa ushahidi na hivyo hawaoni sababu ya kuendelea na mashtaka ya udhalilishaji na ubabe dhidi ya Giggs.
Wakili wa Giggs, Chris Daw alisema mteja wake amepata faraja kwa hatua hiyo na sasa atakuwa na amani baada ya kujikuta katika mapambano kwa takriban miaka mitatu akipambana kusafisha jina lake.
Katika moja ya utetezi wake, Giggs aliwahi kukiri kwamba amewahi kumsaliti mpenzi wake mara kadhaa lakini hakuwahi hata mara moja kumpiga.

Katika miaka yake 23 ya soka la ushindani, Giggs ameichezea Man United katika mechi zaidi ya 900 na kushinda mataji 13 ya Ligi Kuu England (EPL) pamoja na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya kuandamwa na kesi ya udhalilishaji, Novemba mwaka jana Giggs alitangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ukocha kwenye timu ya Taifa ya Wales.
Giggs alisema kwamba alichukua uamuzi huo kwa kuwa hakutaka kesi hiyo iathiri kwa namna yoyote maandalizi ya timu hiyo iliyokuwa ikijiandaa kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar kati ya Novemba na Desemba 2022.
