Na Hassan Kingu
Mashabiki Yanga wamemjadili sana Jonas Mkude ‘Nungunungu; kama anafaa au hafai katika timu hiyo lakini kwa sasa nadhani imetosha, tumuachie kocha Miguel Gamondi afanye maamuzi kwenye kikosi chake.
Tetesi za Simba kuachana na Mkude zikiwa zimepamba moto, zikaibuka tetesi nyingine za kumhusisha na Yanga, Azam na Singida Fountain Gate, kwamba ni vipi mchezaji huyo atafaa kujiunga na moja ya timu hizo.
Mjadala huo hatimaye ukahamia katika klabu ya Yanga, na unaendelea hadi sasa, mashabiki wa timu hiyo na hata wale wasio wa timu hiyo wanamchambua mchezaji huyo kwa namna mbalimbali.
Nionavyo kumjadili Mkude kwa sasa ni sawa na kumkosea heshima kwa kuwa uamuzi umeshafanyika na ni vyema akasubiriwa ili kuonesha ubora wake kama kweli yuko vizuri au ameisha kama ambavyo baadhi ya watu wanadai.
Wanaojenga dhana kwamba Mkude ameisha wanasimamia katika hoja ya mchezaji huyo kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha Simba kwamba klabu hiyo isingekuwa tayari kumuona anaondoka kama bado yuko katika ubora wake.
Wanaosimamia hoja hiyo hawajui au hawataki kukubali kwamba mchezaji huyo huyo anaweza kupata nafasi timu nyingine na kuonesha uwezo.
Hawataki kukubali kwamba mchezaji anaweza kupewa nafasi ya pili akadhihirisha ubora wake baada ya kocha kuamua kumtumia ama kwa kumbadili nafasi anayocheza au kumpanga na wachezaji ambao watamfanya awe tishio.
Katika mjadala wa Mkude nimeona mahali mitandaoni akifananishwa na Juma Kaseja aliyetoka Simba kwenda Yanga lakini hakuwa katika ubora uliozoeleka Simba, hapo hapo pia nilisoma mwingine akimtaja Ibrahim Ajibu kwamba hakuweza kuonesha ubora.
Wanaosimamia hoja hiyo hawajarudi nyuma wakamtaji Yusuf Ismail Bana, beki aliyetoka Simba akaenda Yanga na kuwa tishio, akaitawala beki ya kulia kwa muda mrefu.
Hawamtaji Zamoyoni Mogela, aliyetamba Simba na kuhamia Yanga akicheza vizuri eneo tofauti na kuwa tishio kiasi cha kubatizwa jina la DHL nchini Uganda.
Watu hao hao hawamtaji Method Mogela aliyetoka Simba na ubora wake na kuendelea na ubora huo huo katika kikosi cha Yanga lakini pia hawamtaji Hamis Gaga aliyetoka Simba akilalamikiwa kwa kuwa na tabia zisizopendeza lakini akiwa Yanga akaendeleza makali yake.
Nimetoa mifano hiyo kwa lengo la kuwataka wote wanaomshambulia Jonas Mkude kuacha kufanya hivyo, badala yake waheshimu uamuzi uliofanywa, wamuachie kocha afanye kazi yake, waamini kwamba mchezaji huyo naye bado ana nafasi ya kutamba.
Mwisho wa yote, ni miguu ya Mkude au Nungunungu ndiyo itakayotupa jibu, tuiache ‘izungumze’ na katika hilo tusiwe na haraka, muda utatupa jibu kama miguu ya Mkude ilipaswa kuwa Yanga au Yanga imekurupuka.
Vinginevyo kwa sasa hakuna maana yoyote kuanza kumjadili mchezaji tena katika namna mbaya wakati huu maamuzi yakiwa tayari yameshafanyika, ni mjadala unaoagawa mashabiki na kumkatisha tamaa mchezaji na kimsingi hauna maana yoyote.
Soka Tuipe nafasi miguu ya Mkude izungumze
Tuipe nafasi miguu ya Mkude izungumze
Read also
