Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga leo Alhamisi imetangaza kuingia makubaliano ya udhamini na Benki ya CRDB katika shughuli zote za Wiki ya Mwananchi ambayo itafanyika Julai 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika siku hiyo Yanga itashuka kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kabla ya keshokutwa kuizindua rasmi wiki hiyo jijini Mwanza kwenye Uwanja wa Furahisha.
Imeelezwa siku ya uzinduzi huo kutakuwa na matukio mbalimbali ya kijamii na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa Hip Hop, William Lyimo ‘Billnass’ na Fareed Kubanda ‘Fid Q’.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine mbali na kueleza makubaliano ya mkataba huo utakaosimamia shughuli zote za Yanga lakini pia aliwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo.
“Ni siku muhimu sana kwa kuingia makubaliano na Benki ya CRDB kwa kufanikisha sherehe zetu za Wiki ya Wananchi itakayofunguliwa rasmi Jumamosi hii kule Mwanza ambako tunaenda kufungua rasmi wiki hii.
“Niwashukuru CRDB kwa kuwa sehemu ya kufanikisha jambo hili la furaha lakini pia nawaomba mashabiki wa Yanga waje mapema kwenye siku ya kilele ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali na jioni kutakuwa na mechi kubwa kati ya kikosi chetu dhidi ya Kaizer Chiefs,” alisema Mtine.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa CRDB, Stephen Adili alisema wanaendelea kufanya ushirikiano na Yanga kutokana na ukubwa wao ambao utawasaidia kuwafikia wateja wengi zaidi na wananchi watafanikisha malengo yao katika kupiga hatua katika soka.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema wanaendelea kuimarisha kikosi chao kwa kutambulisha wachezaji wapya ambapo hadi sasa nyota watatu wameshatambulishwa huku akieleza mchezaji mpya mkubwa ambaye wamemsajili atatambulishwa wiki ijayo.
Yanga tayari imetangaza kuwasajili Fred Gift raia wa Uganda kutoka SC Villa ya kwao, Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate na Jonas Mkude aliyekuwa Simba SC.
Soka CRDB mdhamini Wiki ya Mwananchi
CRDB mdhamini Wiki ya Mwananchi
Read also