Na mwandishi wetu
Baada ya Yanga SC juzi kutangaza usajili wa beki wa kati wa Uganda, Gift Fred kutoka SC Villa, imeelezwa usajili huo umemuwashia taa nyekundu beki Mamadou Doumbia (pichani) anayetajwa hatakuwemo kwenye kikosi cha msimu ujao.
Doumbia, beki wa Mali aliyesajiliwa kwa mbwembwe wakati wa dirisha dogo la usajili Desemba, mwaka jana akitokea Stade Malien, alishindwa kumshawishi kocha aliyetangulia, Nasreddine Nabi kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo akionekana ana uwezo wa kawaida.
Beki huyo mrefu aliyetajwa kuwa mahiri kwa mipira ya vichwa alishindwa kufua dafu mbele ya mabeki wazawa nahodha Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca ambao walikuwa wakibadlishana kwenye nafasi ya beki wa kati.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio leo Jumatano Ofisa Habari wa Yanga, katika kinachoonekana kumpa mkono wa kwa heri Doumbia, alisema wanaleta wachezaji wenye uwezo unaolingana kwenye kila nafasi na lengo ni timu kunufaika kutokana na ushindani wa namba.
“Hata sasa ukiona kuna kipa amesajiliwa maana yake kipa mmoja lazima aondoke. Tunasajili wachezaji wenye uwezo kwenye kila nafasi ili timu inufaike kutokana na ushindani wa namba. Sasa kama kuna mmoja katika nafasi anashindwa kuwapa changamoto wenzake, huyo hastahili kuendelea kuwepo Yanga,” alisema Kamwe alipokuwa akizungumzia ujio wa Gift.
Katika mahojiano hayo Kamwe aliorodhesha mabeki wa kati wa Yanga ambao wanatarajia kugombania nafasi na Fred msimu ujao lakini katika hali ya kushangaza hakulitaja jina la Doumbia na kuwa muendelezo wa kinachoaminika beki huyo wa Mali amepewa mkono wa kwa heri.
“Tumemleta Gift Fred kuwapa changamoto zaidi mabeki wetu wa kati Job, Mwamnyeto na Bacca,” alinukuliwa Kamwe akisema bila kumtaja Doumbia.
Soka Gift amuweka pagumu Doumbia
Gift amuweka pagumu Doumbia
Read also
