London, England
Kocha mpya wa Tottenham Hotspur, Ange Postecoglou amesema anataka mshambuliaji, Harry Kane anayewindwa na Bayern Munich abaki katika timu hiyo ingawa bado hajapewa uhakika wa jambo hilo.
Habari za ndani zinadai kwamba Kane ambaye mkataba wake na Spurs unafikia ukomo mwakani ameshaarifiwa kwamba hauzwi lakini mwenyewe anadaiwa kutaka kusaka changamoto mpya nje ya timu hiyo.
Awali Kane alikuwa akiwindwa na klabu za PSG, Real Madrid, Man United ambayo baadaye ilijitoa pamoja na Bayern Munich ambayo tayari imetangaza kuwa tayari kutoa Pauni 70 milioni.
Akizungumza katika mkutano wa kwanza na waaandishi wa habari tangu ajiunge na Spurs, Postecoglou, alisema Kane ni mchezaji muhimu na angependa awe naye katika safari ya mafanikio ya Spurs.
“Harry tayari ni mtu muhimu katika historia ya klabu hii, ni mmoja wa wachezaji bora duniani, nataka aendelee kuwa hapa na nataka kuipa mafanikio klabu hii, naamini na yeye anataka hivyo hivyo,” alisema kocha huyo.
Jumatano hii Kane anatarajia kuanza mazoezi na kikosi cha Spurs kujiandaa na msimu mpya wa 2023-24 na Postecoglou alisema kwamba angependa kuzungumza na mshambuliaji huyo.
“Ninachotaka ni kujitambulisha na nataka afahamu ninachohitaji kifanyike ili kuifanya hii klabu ya soka iwe na mafanikio na baada ya hapo tutaenda mazoezini,” alisema Postecoglou.
Postecoglou alipewa majukumu ya kuinoa Spurs Juni mwaka huu baada ya Antonio Conte kutimuliwa, awali alikuwa akiinoa Celtic ya Scotland ambayo katika msimu wa 2022-23 aliiwezesha kutwaa mataji ya ligi kuu, taji la ligi na taji la Scotland.