Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imetajwa kukamilisha usajili wa beki wa kimataifa raia wa Uganda, Gift Fred (pichani) aliyesaini mktaba wa miaka mitatu akitokea SC Villa ya Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka uongozi wa Yanga, zinaeleza kuwa beki huyo anatarajiwa kuwasili nchini mapema wiki ijayo kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya taratibu na kutambulishwa rasmi kama inavyofanyika kwa wachezaji wengine wapya.
“Tumemalizana na Gift na ni pendekezo la kocha wetu Miguel Gamondi, katika kuangalia mechi zetu za msimu uliopita hasa kwenye mechi za kimataifa alibaini mapungufu kwenye eneo hilo ndio maana akapendekeza tusajili beki wa kati ili kuimarisha eneo hilo,” kilisema chanzo hicho.
Aidha, Mtandao wa Kawowo Sports wa nchini Uganda unaeleza kuwa Yanga wamekamilisha dili hilo wakimpata bure mchezaji huyo baada ya kumaliza mkataba wa kuitumikia Villa.
Taarifa ya mtandao huo inaeleza kuwa mbali na Gift kuwa mhimili mkuu katika eneo la ulinzi la Villa lakini pia beki huyo ameichezea timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ mechi tano tangu alipoanza kuitwa kwenye timu hiyo Januari, mwaka huu.
Kutua kwa beki huyo kunaongeza ushindani wa nafasi ya kucheza katika eneo la beki wa kati kwa Yanga ambalo msimu uliopita, nahodha Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ Dickson Job na Yannick Bangala ndio waliokuwa wanahudumu kwa kupishana.
Hapo hapo zipo habari kwamba Mamadou Doumbia naye anaendelea kuzoea mazingira ya kikosi hicho baada ya kuwa na wakati mgumu msimu uliopita.
Soka Beki SC Villa asajiliwa Yanga
Beki SC Villa asajiliwa Yanga
Read also
