Na mwandishi wetu
Wakati dirisha la usajili Ligi Kuu NBC likifunguliwa rasmi kesho Jumamosi, Julai Mosi, 2023, uongozi wa timu ya KMC umetenga kiasi cha Sh bilioni moja kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya.
KMC imefikia hatua hiyo ili kukiboresha kikosi chao kuanzia msimu ujao ikieleza kutofurahishwa na mwenendo wa timu hiyo katika misimu miwili iliyopita.
Katika msimu wa 2021-22, timu hiyo kutoka Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ilimaliza ligi katika nafasi ya 10 kabla ya msimu uliopita wa 2022-23 kulazimika kucheza mechi za mtoano kuwania kubaki katika ligi hiyo kwa msimu wa 2023-24.
Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala (pchani) amesema kuwa wanahitaji kuwa wa tofauti kuelekea msimu ujao na zaidi wanahitaji wachezaji mahiri kwa ajili ya kuongeza makali zaidi kwa timu hiyo.
“Msimu ujao hatutaki kuona kama yaliyotokea msimu uliomalizika, ndiyo maana tumeamua kuongeza bajeti yetu ya usajili na kufikia Sh bilioni moja, na hatutasubiri mchezaji aachwe kwingine na sisi tumsajili bali tukimuona mchezaji anatufaa, tutakwenda kuvunja mkataba kwa waajiri wake na kumsajili,” alisema Christina.
Pia imeelezwa kuwa kufikia bajeti hiyo, KMC imeongeza kiasi cha Sh milioni 300 kutoka milioni 700 ya bajeti yao ya usajili ya msimu uliopita, ikihitaji kuongeza ushindani katika ligi hiyo inayotajwa kuwa ni ya tano kwa ubora barani Afrika kwa sasa.
Wakati ikipigania kubaki Ligi Kuu NBC katika mechi zake za mwisho za msimu wa 2022-23, KMC ilimuajiri kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye aliiongoza vyema katika mechi za mtoano.
Katika taarifa ya TFF iliyopatikana leo Ijumaa, imeeleza kuwa kipindi cha usajili kitaanza rasmi Julai Mosi na kufungwa Agosti 31.
