Na mwandishi wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewapongeza mabondia Karim Mandonga, Hassan Mwakinyo, wanariadha Alphonce Simbu, Gabriel Geay na klabu za Yanga na Simba kwa mafanikio yao ya mwaka 2023.
Akitangaza kuahirisha vikao vya Bunge mjini Dodoma leo Jumatano, Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hamasa kubwa ambayo amekuwa akiitoa kwenye michezo.
Akiwazungumzia wanariadha hao, Waziri Mkuu alimpongeza Geay kwa kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Boston Marathon wakati Simbu yeye alipongezwa pia kwa kushika nafasi ya pili katika Osaka Mrathon na Guanzou Half Marathon.
Kuhusu klabu za Yanga na Simba, Waziri Mkuu aliipongeza Yanga kwa kufikia kwa mara ya kwanza hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na Simba kwa kufikia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabondia wengine waliopongezwa na Waziri Mkuu kwa mafanikio yao ni Twaha Kiduku, Ibra Classic, Mfaume Mfaume, Seleman Kidunda pamoja na bondia mwanamke Fatma Yazidu aliyemtwanga bondia wa Kenya, Consolata Msanga.
Waziri Mkuu pia aliipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa, vyombo vya habari pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kukuza michezo nchini.
Kuhusu TFF, Waziri Mkuu alisema Ligi Kuu ya Tanzania inazidi kupata umaarufu ikiwa nafasi ya tano Afrka lakini pia alilipongeza shirikisho hilo kwa mafanikio yanayoonekana ya Taifa Stars inayopambana katika michuano ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika.
Sports Mix Waziri Mkuu awapongeza Yanga, Mandonga, Geay
Waziri Mkuu awapongeza Yanga, Mandonga, Geay
Read also