Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeeleza kuwa imeshakamilisha mchakato wa kuwanasa makocha watatu wapya kwa ajili ya kukamilisha jopo la benchi la ufundi la timu hiyo kwa ajili ya kusaka mafanikio ya msimu ujao.
Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally (pichani) amesema makocha hao wako vizuri kuziba nafasi tatu zilizoachwa wazi na kocha wa makipa, Zakaria Chlouha, kocha wa viungo, Kelvin Mandla na mtaalam wa viungo, Fareed Cassim.
Ingawa meneja huyo hakuwa tayari kubainisha maelezo mengine juu ya kupatikana kwa makocha hao, alisema mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kwani ni makocha wazuri, wenye weledi mkubwa wa utendaji wa kazi zao.
“Kwa sasa tumeshapata wataalamu wote hao watatu kwa maana pia ya kocha wa viungo ambaye yuko vizuri sana, na ubingwa unaanzia kwenye utimamu wa wachezaji, kama una wachezaji legelege maana yake hawatakuwa na uwezo wa kumudu dakika 90 au watakuwa na majeraha kila wakati,” alisema Ally.
Alisema wana imani na makocha hao, wanafahamu kiu ya mashabiki na wapenzi wa Simba ya kuhitaji mafanikio kuanzia msimu ujao hivyo nao wamefanya jambo stahiki katika hilo.
Ally pia alisema kuwa bado wanaendelea na mazungumzo na wachezaji wengine ambao wataachana nao na kwamba hawajamaliza zoezi hilo licha ya kwamba wameshawatema wachezaji saba hadi sasa.
