New York, Marekani
Rapa Big Pokey (pichani) wa Marekani amefariki dunia jukwaani wakati akiwa kwenye onesho la muzuki katika ukumbi mmoja wa burudani Jumapili hii mjini mjini Texas.
Big Pokey mwenye umri wa miaka 48 ambaye jina lake halisi ni Milton Powell mara baada ya kuzidiwa alikimbizwa hospitali kabla ya kubaika kwamba amefariki wakati juhudi za kumpatia matibabu zikiendelea.
Awali Big Pokey alikuwa mmoja wa wasanii waliounda kundi la Screwed Up Click lakini alifahamika zaidi kupitia albamu yake ya kwanza ya ‘Hardest Pit in the Litter’ iliyotoka mwaka 1999.
Baada ya hapo, Big Pokey aliendelea kukimbiza kwenye gemu na kufanikiwa kutoa albamu tano ikiwamo ya hivi karibuni ya ‘Sensei’ aliyoitoa mwaka 2021.
Awali taarifa za kifo cha Big Pokey zilitolewa na rapa mwenzake Bun B ambaye alitumia mtandao wa Instagram kutoa taarifa za kifo hicho.
“Mmoja wa wasanii wenye kipaji asili mjini, asiye na makuu, mtu muungwana ambaye anakwenda na utu na heshima zake, ni mtu rahisi kumpenda na vigumu kumchukia,” alisema Bun B akimpamba Big Pokey kabla ya kuuarifu umma kwamba mtu huyo amefariki dunia.
