Budapest, Hungary
Kocha wa Roma, Jose Mourinho amefungiwa mechi nne na Uefa kwa kosa la kumzonga mwamuzi Anthony Taylor na kumtolea lugha kali baada ya mechi ya fainali ya Europa Ligi dhidi ya Sevilla.
Mourinho anadaiwa kumtolea lugha kali mwamuzi huyo wakati wa mechi na baada ya mechi inadaiwa alimvaa na kumbughudhi kwenye eneo la kuegesha magari akidaiwa kutofurahishwa na maamuzi ya Taylor katika mechi hiyo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Budapest, baada ya sare ya bao 1-1, Roma ililala kwenye mikwaju ya penalti ambapo Mourinho anadaiwa kutumia lugha kali au za kudhalilisha kwa Taylor.
Sambamba na adhabu aliyopewa Mourinho, klabu zote mbili zimepewa adhabu tofauti tofauti kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu yaliyofanywa na wachezaji na mashabiki wao katika mechi hiyo.
Mourinho katika mechi hiyo alipewa kadi ya njano lakini pia alimpa wakati mgumu mwamuzi wa akiba ambaye alilazimika mara kadhaa kumtuliza kocha huyo aliyeonekana kujawa hasira kwa muda mrefu.
Roma imepigwa marufuku kuuza tiketi na mashabiki wake kusafiri katika mechi za Ulaya za msimu ujao na kutozwa faini ya Pauni 47,000 kwa kosa la kurusha vitu mbalimbali uwanjani na kulipua baruti.
Katika mechi hiyo, Taylor alilazimika kutoa kadi za njano 13 kwa wachezaji mbalimbali ikitajwa kuwa ni rekodi ya kutolewa kadi nyingi katika mechi ya Europa Ligi, saba kati ya hizo wakipewa wachezaji wa Roma.
Mourinho mbali na kumtolea lugha kali na kumbughudhi Taylor pia hakuifurahia medali aliyopewa baada ya timu yake kushika nafasi ya pili, badala yake hapo hapo akaigawa medali hiyo kwa shabiki mmoja kijana.
Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo, kocha huyo alisema kwamba yeye huwa hahifadhi medali hizo badala yake huhifadhi zile za dhahabu anazopewa mshindi.
Kwa adhabu alizopewa, Mourinho sasa atazikosa mechi nne za mwanzo za Europa Ligi kwa kuwa timu yake yake imefuzu michuano hiyo baada ya kushika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu Italia au Serie A.
Kimataifa Mourinho afungiwa mechi nne
Mourinho afungiwa mechi nne
Read also
