Na mwandishi wetu
Timu ya Mashujaa FC ya Kigoma imetua jijini Mbeya alfajiri ya kuamkia Jumatano hii, wakiwahi mapema kwa ajili ya maandalizi kabambe kabla ya mechi ya marudiano na Mbeya City itakayopigwa Juni 25, mwaka huu.
Mashujaa iko mbele kwa ushindi wa mabao 3-1, ushindi ilioupata Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, ikihitaji sare au kutofungwa mabao zaidi ya 2-0 ili kushiriki Ligi Kuu NBC msimu ujao.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdul Mingange (pichani) amezungumza na GreenSports na kusema wamefika salama Mbeya na hawahitaji kufahamika wameweka kambi wapi ili wapate utulivu stahiki wakiwa wanajipanga kuelekea mechi hiyo.
“Ni mchezo mgumu kwao na kwetu pia, sisi tunataka kushinda twende Ligi Kuu na wao wanataka kubadili matokeo wakiwa kwao kwa hiyo nasi tunajipanga tukilifahamu hilo, tukijua kibarua kikubwa kipo mbele yetu ndiyo maana tumefika hapa mapema, tumefika tangu alfajiri ya kuamkia leo.
“Vijana wamewaona wapinzani wetu kwenye mechi iliyopita na sisi benchi la ufundi tumeona kwa hiyo tutashirikiana kuhakikisha tunasuka mipango na tunaingia kwa kutazama nini kinaendelea ndani ya mchezo ili tufanikishe azma tuliyonayo,” alisema Mingange.
