Manchester, England
Klabu ya Barcelona imefikia makubaliano na Manchester City ya kumsajili kiungo Ilkay Gundogan akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake wa sasa kufikia ukomo Juni 30 mwaka huu.
Gundogan, nyota wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 32, amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili na Barca ambao una kipengele kinachoiruhusu klabu hiyo kuongeza mwaka wa tatu.
Hadi kukubali kujiunga na Barca, Gundogan amekataa ofa ya kuendelea kuichezea Man City akiwa tayari ameichezea timu hiyo kwa miaka saba, lakini pia amekataa ofa ya Arsenal na klabu za Saudi Arabia.
Machi mwaka huu zilikuwapo habari kwamba Barca ilianza mchakato wa kumsajili mchezaji huyo ikidaiwa kwamba kutokana na kanuni za matumizi ya fedha kuwabana, klabu hiyo imeamua kukimbilia kwa mchezaji huyo ili kumsajili akiwa huru.
Kwa upande wa Man City kulikuwa na ugumu kumruhusu kiungo huyo kuondoka ingawa ilichotaka ni kumpa mkataba wa mwaka mmoja lakini mwenyewe akaamua kuichagua Barca licha ya kocha wa Man City, Pep Guardiola kuonesha nia ya kumbakisha katika timu hiyo.
Kocha wa Barca, Xavi ndiye aliyeongoza mpango wa kumsajili Gundogan ili kuiimarisha timu hiyo hasa baada ya kumkosa Lionel Messi ambaye amejiunga na klabu ya Inter Miami ya Marekani.
Kimataifa Gundogan asajiliwa Barca
Gundogan asajiliwa Barca
Read also
