London, England
Kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante (pichani) amekubali kujiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia kwa mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Pauni 86 milioni.
Kante anaungana na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni ambaye pia waliwahi kuwa na Kante kwenye timu ya Taifa ya Ufaransa.
Mchezaji mwingine maarufu anayecheza soka Saudi Arabia ni Cristiano Ronaldo anayeichezea klabu ya Al Nassr ambayo alijiunga nayo Januari mwaka huu.
Kante mwenye umri wa miaka 32 hivi karibuni alikuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na timu hiyo hasa kwa kuwa mkataba wake na Chelsea unafikia ukomo mwishoni mwa Juni mwaka huu.
Mchezaji huyo hata hivyo amekuwa na wakati mgumu ndani ya Chelsea katika msimu huu wa 2022-23 kutokana na kuandamwa na majanga ya kuwa majeruhi akiichezea timu hiyo katika mechi tisa tu.
Baada ya kukubali kujiunga na Al-Ittihad, Kante amehitimisha maisha yake ya soka katika Ligi Kuu England (EPL), atakumbukwa kwa kuiwezesha Leicester City kubeba taji la EPL msimu wa 2016-17.
Akiwa Chelsea, Kante pia atakumbukwa kwa kutoa mchango mkubwa hadi kuiwezesha timu hiyo kutwaa mataji ya EPL, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa na Kombe la FA.
Kante ambaye pia alitoa mchango mkubwa kwa timu ya Taifa ya Ufaransa hadi kubeba Kombe la Dunia mwaka 2018, katika msimu wa 2016-17, alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka na ile ya Chama cha Wanasoka Profesheno.
Kimataifa Kante amfuata Benzema Saudi Arabia
Kante amfuata Benzema Saudi Arabia
Read also
