Nyon, Switzerland
Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin (pichani) ameishauri Saudi Arabia kuwekeza katika akademi, makocha na kukuza vipaji vya ndani badala ya kununua wachezaji mastaa wa Ulaya.
Ceferin alikuwa akijibu swali kuhusu Saudi Arabia kuwa tishio kwa soka la Ulaya kwa namna inavyonunua wachezaji mastaa wa bei mbaya Ulaya badala yake ameliona jambo hilo kuwa ni kosa kama lile lililofanywa na China.
Klabu za Saudi Arabia katika siku za karibuni zimekuwa zikinunua wachezaji mastaa wa Ulaya kwa bei mbaya na kuibua hofu kwamba huenda jambo hilo likaathiri soka la Ulaya jambo ambalo Ceferin amelipinga.
Cristiano Ronaldo, Januari mwaka huu alijiunga na klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia pamoja na nyota mwenzake wa zamani wa Real Madrid ambaye mapema mwezi huu amesajiliwa na klabu ya Al-Ittihad pia ya Saudi Arabia.
Wachezaji wengine wanaotajwa kuwa mbioni kwenda Saudi Arabia ni Ruben Neves wa Wolves na Kalidou Koulibaly wa Chelsea.
“Ni kosa hilo hilo lililofanywa na China, wote wananunua wachezaji ambao wanaelekea mwisho wa maisha yao ya soka la ushindani, wawekeze katika akademi, waajiri makocha na waendeleze wachezaji wa kwao,” alisema Ceferin.
Mpango wa klabu za Saudi Arabia kununua wachezaji wa bei mbaya pia unatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati maalum wa nchi hiyo kukuza ligi yao, kujitangaza na hatimaye kufanikisha azma ya kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2030.
