Na mwandishi wetu
Beki wa Taifa Stars, Novatus Dismas amesema kwamba amekuwa na mafanikio ya kucheza namba tofauti (kiraka) kutokana na kufuata maelekezo maalum ya uchezaji wa nafasi anayopewa kwa wakati husika.
Dismas (pichani) amekuwa akitumika kwenye nafasi mbalimbali za ulinzi na amekuwa akizimudu kama kiungo wa ulinzi, beki wa pembeni kabla ya kuonekana akicheza kwa ufasaha nafasi ya beki wa kati kwenye kikosi cha Stars.
“Kikubwa ninachoanza kuangalia ni maelekezo ya mwalimu, baada ya maelekezo ndiyo unafanya kitu chako cha ziada, huwezi kufanya cha ziada kabla ya maelekezo maana utakwenda tofauti tu sababu timu ni kikundi cha watu, unapofanya mambo yako kwanza unavuruga vitu vingi.
“Unajua walimu wengi wanaamini nina uwezo wa kuanza na timu kama kiongozi kwenye maeneo tofauti kama kiongozi kwa wenzangu ninaocheza nao, kwa hiyo naweza kucheza kokote kutokana na mawasiliano yangu na wachezaji wengine,” alisema Dismas.
Beki huyo anayekipiga Zulte Waregem ya Ubelgiji ameendelea kuwa lulu baada ya juzi akiwa beki wa kushoto wa Stars, kutoa pasi ya bao pekee kwa Simon Msuva, timu hiyo ilipokuwa ikiumana na Niger kuwania tiketi ya kushiriki Afcon 2023.
Dismas amekuwa akitumika Zulte mara nyingi kama beki wa kati au wa kushoto kulingana na mfumo husika lakini akiwa tayari ametumika kama kiungo mkabaji, beki wa kati na kiungo wa kushoto katika timu nyingine za Azam, Alliance, Maccabi Tel Aviv, Beitar Tel Aviv na Biashara United alizowahi kuzitumikia.
