Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Yanga, umemwalika kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ambaye anatajwa kutimkia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Kwa sasa uongozi wa timu hiyo upo katika mchakato wa kusaka mbadala wa Nabi pamoja na kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Rais wa Yanga, Hersi Said alieleza kuwa wameamua kumpa Nabi mwaliko huo kutokana na utaratibu wao wa kuishi kwa upendo na watumishi wao pamoja na mafanikio aliyowapa katika kipindi chote cha misimu miwili na nusu alichokuwa Yanga.
“Huu ni mwaliko maalumu ambao umetoka kwa mfadhili wetu, Ghalib Said na hiyo ni kutokana na kuthamini mchango wake na mafanikio aliyoipa timu yetu na itakuwa fursa pekee kuagana na mashabiki na wanachama ambao walimpenda kutoka moyoni,” alisema Hersi.
Pia inaelezwa kuwa Nabi amekubali mwaliko huo na atahudhuria sherehe hiyo ambayo hutumika kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi kuelekea msimu unaofuata.
Hersi alieleza kuwa wanajivunia mahusiano mazuri waliyokuwa nayo na kocha huyo ambaye kitendo chake cha kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kimeifanya timu hiyo kujulikana zaidi Afrika nzima.
Nabi bado yuko jijini Dar es Salaam na leo Jumanne majira ya saa sita za mchana alionekana katikati ya jiji barabara ya Azikiwe akiwa kwenye pikipiki.
Soka Nabi aalikwa Wiki ya Mwananchi
Nabi aalikwa Wiki ya Mwananchi
Read also
