Na Hassan Kingu
Kocha Nasreddine Nabi ameondoka Yanga, huko anakokwenda iwe Kaizer Chiefs au kwingineko moja ya swali atakaloulizwa ni mahitaji yake kuanzia wachezaji anamtaka nani pamoja na benchi la ufundi.
Na ingawa zimekuwapo habari kwamba hatochukua mchezaji yeyote katika klabu ya Yanga, uongozi Yanga haupaswi kubweteka badala yake ujiandae kwa lolote.
Upo uwezekano, tena mkubwa tu wa kuwapoteza baadhi ya mastaa wake au sehemu kubwa ya wasaidizi wake katika benchi la ufundi la Yanga wakalazimika kuondoka na kocha huyo huko aendako.
Katika benchi la ufundi mhanga wa kwanza anaweza kuwa Cedric Kaze, katika kipindi chote ambacho Nabi amedumu Yanga kuanzia Aprili 2021 hadi Juni 2023, Kaze amekuwa mmoja wa wasaidizi wake muhimu.
Hatujui umuhimu wa Kaze kwa Nabi, anayejua ni Nabi mwenyewe na ndio maana wamekuwa pamoja katika safari ya mafanikio ya Yanga hadi kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kubeba mataji kadhaa nchini,

Kwa hali hiyo tusishangae akaamua kufuatana naye huko anakokwenda, kwa maana nyingine Yanga wasijiaminishe kwa asilimia 100 kwamba Kaze hawezi kuondoka.
Hadithi ya Kaze inaweza kufanana ya Charles Boniface Mkwassa akiwa Yanga kama msaidizi wa Hans Pluijm, kocha huyo alipopata nafasi ya kuinoa timu moja ya Saudi Arabia aliondoka na Mkwasa na ingawa mambo hayakuwa mazuri lakini Pluijm alionesha ni kwa kiasi gani Mkwasa alikuwa mshauri mzuri kwake hivyo tusishangae jambo kama hilo kutokea kwa Kaze na Nabi.
Na kwa Yanga si Kaze peke yake bali Nabi anaweza kuondoka na watu wengine katika benchi la ufundi kuanzia wataalamu wa viungo na wengineo ambao ataona umuhimu wao kwake.
Djigui Diarra

Kwa upande wa wachezaji hapa ndipo kuna mengi, kila mchezaji anataka maslahi, anataka changamoto mpya, anataka fursa ya kuonekana katika ligi ambazo zitamfungulia njia ya kwenda kucheza soka barani Ulaya.
Na hapa bila kupepesa Yanga wasishangae wakipoteza wachezaji wao muhimu, kipa Djigui Diarra, huyu ni namba moja, amedhihirisha uwezo wake si tu katika ligi kwa kubeba tuzo ya kipa bora lakini hata kwenye michuano ya klabu Afrika.
Diarra amekuwa nyota wa mchezo katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya USM Alger na Yanga, amekuwa nguzo muhimu katika safari ya mafanikio ya Yanga katika misimu miwili.
Kilicho wazi ni kwamba hakuna timu au kocha ambaye hapendi kuwa na kipa wa aina ya Diarra. Yanga ijiandae kwa lolote.
Fiston Mayele
Huyu naye ni mchezaji mwingine aliyedhihirisha umahiri na ubora wake, Afrika inatambua ubora wake, ameibuka kinara wa mabao katika Ligi Kuu NBC lakini pia ndiye kinara wa mabao katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Yote haya yanamfanya Fiston Mayele kuwa hazina muhimu ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao lakini hapo hapo kuna ukweli kwamba zipo klabu nyingine zinazomtaka, haitoshangaza Nabi akaungana naye huko anapokwenda.
Kwa Mayele tayari zimekuwapo fununu kwa muda mrefu sasa kwamba anatakiwa Arabuni na hata Afrika Kusini hivyo haitokuwa ajabu akiondoka na kuacha maumivu Yanga kwani ubora wake ni jambo lililo dhahiri.
Yannick Bangala
Amekuwa na tatizo, kuna wakati hawi katika ubora wake lakini jambo hilo haliwezi kuondoa ukweli kwamba Yannick Bangala ni mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya Yanga na ndio maana amekuwa mara kwa mara yumo kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Anayemjua vizuri mchezaji huyo ni Nabi, anajua umuhimu wake na anajua nini cha kufanya ili ayaone matunda ya ubora wa Bangala na kukabiliana na tatizo la kushuka ubora ambalo kuna wakati humtokea.
Na japo Bangala hapewi nafasi kubwa sana ya kuondoka Yanga lakini mabosi wa klabu hiyo wajiandae lolote linaweza kutokea kwani kama nilivyosema awali kwamba anayeujua vizuri ubora na udhaifu wa Bangala ni Nabi na anajua nini cha kufanya kwa mchezaji huyo.
Kennedy Musonda
Mfungaji wa bao lililoipa Yanga taji la FA (ASFC) naye ni mtu mwingine muhimu katika kikosi cha Yanga, amekuwa katika ubora ambao umeibeba klabu mara kadhaa, na ndio maana ni mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Musonda ana kila kitu cha kumfanya amudu kucheza kwenye ligi yoyote ya soka barani Afrika na ndio maana yupo Tanzania akiwa mmoja wa wachezaji kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.
Nabi anaujua umuhimu wa Musonda lakini Nabi ameondoka Yanga hivyo hiyo haitokuwa ajabu akiungana na mchezaji huyo huko aendako.
Mudathir, Sure Boy
Mafundi hawa wawili Salum Aboubakar ‘Sure Boy na Mudathir Yahya, wanahitaji pongezi, wote walikuwa Azam lakini tangu watue Yanga wameweza kuteka hisia za mashabiki si tu wa timu hiyo bali wadau wa soka kwa ujumla.
Kwanza wameweza kupenya katika kikosi cha kwanza chenye timu iliyosheheni mastaa kutoka sehemu mbalimbali Afrika, hili ni jambo linalohitaji pongezi, si wachezaji wengi wa Kibongo wenye uwezo huo.
Kitendo cha Nabi kuwa tayari kuwachukua wachezaji ambao walionekana kama kususwa na kutopewa umuhimu katika timu nyingine kinafikirisha, katika hali ya kawaida mtu anaweza kujiuliza unachukuaje mchezaji asiyehitajika anakotoka.
Kocha Nabi aliyajua tusiyoyajua wengi kwa Mudathir na Sure Boy na hilo limejionesha kwa namna ambavyo amekuwa akiwatumia katika kikosi chake, ni kati ya wachezaji ambao umuhimu wao Yanga ni jambo lililo wazi.
Jambo zuri kwa Sure Boy na Mudathir ni kwamba wakianza kipindi cha kwanza utaona umuhimu wao na hata wakiingia kutokea benchi utaliona jambo hilo. Nani atashangaa mmoja wao au wote wakiungana na Nabi huko aendako?
Fei Toto
Maumivu ambayo huenda yakawakuta Yanga kwa wachezaji wao kumfuata Nabi, Azam nao wajiandae, wanaweza wasiwe salama, Feisal Salum au Fei Toto ni mtu mwingine aliyekuwa muhimu mno katika kikosi cha Nabi Yanga.

Ile hadithi ya No Fei No Problem (Hakuna Fei hakuna tatizo) ni mazungumzo tu ya kujifariji, ukweli ni kwamba Fei Toto alikuwa mchezaji muhimu na aliyehitajika katika kikosi cha Yanga.
Alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza Yanga chini ya kocha Nabi, na ndio maana kutokana na ubora wake Yanga waliumia mno aliposusa Desemba mwaka jana na pengine baadhi yao bado wana hasira kwa kitendo hicho hata baada ya mchezaji huyo kuhamia rasmi Azam FC.
Nabi akipata fursa ya kumsajili Fei au akiwa na uhitaji wa mchezaji katika eneo analochezea Fei, mmoja wa wachezaji ambao atawaingiza katika hesabu za kuwasajili ni Fei, hatoona tabu kumchukua mchezaji huyo na kuungana naye kwa mara nyinngine.
Nimewataja wachezaji wachache lakini kimsingi klabu ya Yanga au hata Simba zijiandae kwa lolote, zinaweza kupoteza baadhi ya wachezaji wao muhimu kuungana na Nabi huko aendako kwani anaijua ligi ya Tanzania na anawajua mastaa wenye uwezo.
Takwimu zinazoibeba ligi ya Tanzania na kuitaja kuwa ni ligi bora namba tano Afrika zinamaansha kwamba katika ligi hiyo kuna wachezaji bora ambao pia wanahitajika kwingineko.
