Na mwandishi wetu
Baadhi ya wachezaji wa Simba wanahesabu siku ili kujua hatma yao iwapo watasalia kwenye timu hiyo au watatemwa na kimsingi wamebakiza saa zisizozidi 48.
Habari iliyothibitishwa hivi karibuni ni kuwa panga litapita katika klabu hiyo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo ambapo uongozi utakuwa umemaliza taratibu zote za kuachana na wachezaji hao.
Msemaji wa Simba, Ahmed Ally leo Ijumaa amenukuliwa akisema kuwa ripoti ya kocha wao mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ imetaka wachezaji hao kuachwa na kusajiliwa wenye uwezo mkubwa.
Alisema kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Simba hivi karibuni kilifanya uchambuzi na tayari uongozi umefanya mazungumzo na wachezaji husika hasa wale ambao bado wana mkataba ili kumalizana nao salama.
“Kupitia ripoti ya kocha Robertinho tumepitia kuangalia anataka nini, imejadiliwa na kuchambuliwa. Ameainisha wachezaji baadhi tuachane nao, na wengine bado wana mikataba. Lazima tuzungumze nao tuangalie namna ya kukubaliana nao,” alisema Ally.
Miongoni mwa wachezaji waliotajwa kwenye tetesi za kuachwa kwa muda mrefu ni Gadiel Michael, Joash Onyango, Nelson Okwa, Jonas Mkude, Ismail Sawadogo, John Bocco na Mohammed Ouattara huku aliyetangazwa kuachwa mpaka sasa akiwa ni Augustine Okrah.
Pia wapo wanaotajwa kuwa watapelekwa kwenye klabu nyingine na moja ya klabu inayotajwa ni ile ya West Armenia iliyoingia nao ushirikiano hivi karibuni na kwa mujibu wa Ally, wakishaachana na wachezaji waliopendekezwa wataanza kutangaza usajili mpya.
Tayari usajili unaotajwa kukamilika ni wa winga Mcameroon, Leandre Onana na sasa wanatazamwa wachezaji wengine waliopendekezwa na benchi la ufundi huku Ally akisisitiza pia wako mbioni kulisuka vilivyo benchi lao la ufundi baada ya jana kutangaza kuachana na baadhi ya watendaji wake.
“Msimu ujao tuna malengo makubwa, lazima uambatane na watu wenye malengo kama hayo na sasa tupo sokoni kutafuta wataalam wengine bora zaidi,” alisema.
Makocha waliotemwa ni aliyekuwa kocha mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula, mtaalam wa viungo, Fareed Cassim, kocha wa viungo Kelvin Mandala na kocha wa makipa, Chlouha Zakaria.
