Na mwandishi wetu
Kitendawili cha mfungaji bora Ligi Kuu NBC kimeteguliwa kwa Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza wote kupewa tuzo hiyo baada ya kila mmoja kufunga mabao 17 na wote wameng’ara kwa kubeba tuzo nyingine mbili.
Vinara wengine wa soka waliong’ara kwa ufungaji na kushinda tuzo ni Jentrix Shikangwa wa Simba Queens ambaye kama ilivyo kwa Mayele na Ntibazonkiza naye amemaliza Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na mabao 17.
Naye mshambuliaji wa Ihefu, Andrew Simchimba yeye amebeba tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Kombe la FA (ASFC).
Hafla ya utoaji tuzo hizo ilifanyika Jumatatu hii usiku mjini Tanga ambapo awali zilikuwapo hisia miongoni mwa wadau wa soka kwamba TFF ingekuja na kigezo cha kumpa tuzo mfungaji bora mmoja kati ya Mayele au Ntibazonkiza.
Wachezaji hao mbali na kutwaa tuzo ya mfungaji bora, kila mmoja ana tuzo nyingine mbili, Mayele ana tuzo ya bao bora la msimu na ile ya mchezaji bora wa msimu wakati, Ntibazonkiza naye pia ana tuzo ya fair play na kiungo bora.

Sambamba na tuzo hizo, Mayele na Ntibazonkiza pia wamo kwenye kikosi bora cha msimu wa 2022-23 ambao pia umehitimishwa Jumatatu hii kwa mechi ya fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Azam, mechi iliyoisha kwa Yanga kuifunga Azam bao 1-0.
Ukiachana na wachezaji hao, kipa wa Yanga, Djigui Diarra yeye ametwaa tuzo mbili akiwa na tuzo ya kipa bora wa ASFC pamoja na ya Ligi Kuu NBC na yumo pia kwenye kikosi bora cha msimu.
Wachezaji wengine wa Yanga, beki Dickson Job amebeba tuzo ya beki bora wakati Bakari Mwamnyeto amebeba tuzo ya mchezaji bora wa ASFC na wote hao wameingia kwenye kikosi bora.
Katika kikosi bora cha msimu pia wamo Mohammed Hussein, Henoc Inonga, Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe na Clatous Chama ambao wote ni wachezaji wa Simba wakati kocha wa Yanga, Nasredinne Nabi yeye ametwaa tuzo ya kocha bora.

Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ameshinda tuzo ya mchezaji bora kijana chini ya miaka 20 anayecheza ligi kuu wakati Lameck Lawi wa Coastal Union ameshinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi katika ligi hiyo hiyo.
Kwa upande wa ligi ya Championship mchezaji bora wa ligi hiyo ni Edward Songo wa JKT Tanzania wakati meneja bora wa uwanja ni Omar Malule na tuzo ya gwiji wa zamani wa soka imekwenda kwa Leopold Mukebezi beki wa zamani wa timu ya Pan Africa na Taifa Stars.
Tuzo ya mwamuzi bora wa ligi hiyo imechukuliwa na Jonesia Rukyaa wakati ile ya mwamuzi msaidizi imebebwa na Frank Komba huku Jonesia Rukya, Zawadi Yusuph, Athuman Rajab na Ally Simba wakibeba tuzo ya seti bora ya waamuzi kwa namna walivyosimamia vizuri mechi ya Geita Gold na Dodoma Jiji na Isack Munisi amebeba tuzo ya kamishna bora.
Kwa upande wa WPL mbali na Jentrix (pichani juu) aliyetwaa tuzo ya mfungaji bora, Ally Ally wa JKT Queens ametwaa tuzo ya kocha bora wakati Donisia Minja akitwaa tuzo ya mchezaji bora, Winfrida Charles tuzo ya mchezaji bora chipukizi na Najat Abbas yeye amechukua tuzo ya kipa bora.
Katika WPL pia, tuzo ya mwamuzi bora imekwenda kwa Ester Adalbert wakati ile ya mwamuzi msaidizi imechukuliwa na Glory Tesha.
