Na mwandishi wetu, Tanga
Yanga imezima ndoto za Azam kubeba taji msimu huu baada ya kuichapa bao 1-0 katika mechi ya fainali ya Kombe la FA (ASFC) iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga, leo Jumatatu.
Kwa ushindi huo Yanga sasa imemaliza msimu na mataji mawili baada ya kubeba lile la Ligi Kuu NBC na sasa timu hiyo inajiandaa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wakati Azam itaangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kennedy Musonda ndiye aliyeacha kilio Azam baada ya kufunga bao hilo pekee katika dakika ya 16 kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Tuisila Kisinda au TK Master.
Dakika nne baada ya kuingia bao hili, Musonda nusura aipatie Yanga bao la pili baada ya kuinasa pasi ya Benard Morisson na kufumua shuti ambalo hata hivyo lilitoka nje.
Dakika saba baada ya Musonda kukosa bao, Azam walijibu mapigo na kufanya shambulizi lililozaa mpira wa adhabu baada ya Khalid Aucho kumchezea rafu James Akaminko lakini shuti lililopigwa na Ayoub Lyanga lilidakwa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra.

Dakika 10 kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, Yanga nao walipata mpira wa adhabu baada ya Kisinda ambaye baadaye alitolewa na kuingia Mudathir Yahya, kuchezewa rafu lakini shuti la Morisson halikuweza kuipatia bao timu hiyo.
Makocha wa timu zote walifanya mabadiliko katika mchezo huo lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuleta matokeo tofauti kwani hadi mwisho wa mchezo Yanga walitoka uwanjani na bao lao moja lililowawezesha kubeba kombe.
Yanga inakuwa imelibeba taji hilo kwa mara ya pili mfululizo, ikifanya hivyo msimu uliopita ilipokutanana Coastal Union katika hatua ya fainali na kushinda kwa penalti 4-1 baada ya sare ya mabao 3-3.
